Rekodi tatu alizoweka Welbeck, Man United ikichapwa EPL
Muktasari:
- Ushindi huo ulikuwa ni wa nne kwa Brighton dhidi ya Man United katika mechi tano za mwisho walizokutana kwenye Ligi Kuu ya England (EPL)
Brighton. Brighton iliendeleza ubabe wake dhidi ya Manchester United jana ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani huku nyota wake Danny Welbeck akiandika rekodi mbili.
Ushindi huo ulikuwa ni wa nne kwa Brighton dhidi ya Man United katika mechi tano za mwisho walizokutana kwenye Ligi Kuu ya England (EPL), shukrani kwa mabao ya Danny Welbeck na Joao Pedro huku lile la Manchester United likifungwa na Amad Diallo.
Welbeck alitangulia kuipatia bao, Brighton katika dakika ya 32 akimalizia pasi ya Kaoru Mitoma lakini Diallo aliisawazishia Man United katika ya 60 akimalizia pasi ya Noussair Mazraoui na aliyeifanya mechi hiyo isimalizike kwa sare ni Joao Pedro ambaye alipachika bao la ushindi la Brighton katika dakika za majeruhi.
Hata hivyo kivutio kilikuwa ni bao la Welbeck ambalo limemfanya mshambuliaji huyo kuweka rekodi tatu tofauti.
Rekodi ya kwanza ni kufikisha idadi ya mabao 100 ambayo amepachika tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa ambayo ni ya kwake binafsi.
Ukiondoa rekodi hiyo, Welbeck pia ameweka rekodi nyingine mpya ya kuwa mchezaji wa kwanza wa zamani wa Manchester United kuifunga timu hiyo mabao matano katika Ligi Kuu.
Kabla yake hakuna mchezaji yeyote aliyewahi kuichezea timu hiyo aliyewahi kuifungia mabao matano au zaidi kwenye EPL kama ambavyo Welbeck alifanya jana.
Mshambuliaji huyo pia ameweka rekodi nyingine ya tatu ambayo ni ya kufunga bao katika misimu 15 mfululizo aliyocheza katika Ligi Kuu England ambayo inamfanya adhihirishe kuwa ni miongoni mwa wachezaji wenye muendelezo mzuri kwenye ligi hiyo.
Na idadi kubwa ya mabao ambayo Welbeck ameyafunga ameyapata wakati alipokuwa akizichezea Manchester United na Arsenal kwa nyakati tofauti.
Welbeck aliichezea Manchester United idadi ya mechi 149 na kuifungia mabao 29 huku akifunga idadi ya mabao 32 katika mechi 126 ambazo aliichezea Arsenal na mengine alipachika akiwa anazitumikia timu za Sunderland, Watford, Preston na Brighton.