Prime
Ratiba mpya EPL Chelsea, Liverpool zabananishwa
LONDON, ENGLAND. UTAMU umeshawekwa mezani. Wakati ikiwa zimepita wiki kadhaa tu tangu kumalizika kwa Ligi Kuu England, tayari ratiba mpya ya msimu ujao wa 2023/24 imeshatoka huku mchezo wa kwanza baina ya Liverpool na Chelsea ndio ukionekana kusubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu zote hizo.
Ratiba mpya inaonyesha mechi zitaanza kupigwa Agosti 11, 12, 13 na 14 ambapo timu nyingi zitashuka dimbani Agosti 12 itakapopigwa michezo sita.
Mchezo wa Liverpool na Chelsea unatarajiwa kupigwa katika dimba la Stamford Bridge, Agosti 13, saa 12:30 jioni utakuwa ni wakutafuta mbabe wa kwa sababu msimu uliopita zote zilimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Timu ambazo zimekutana mara 194 kwenye michuano tofauti tofauti, historia zao zinaonyesha kwamba Liverpool ndio mbabe kwani imeshinda mechi 84, 45 zikamalizika kwa sare na Chelsea ikashinda 65.
Chelsea itakuwa inatazamia kurudi kwenye mstari baada ya kufanya vibaya sana kwa msimu uliopita ambapo ilimaliza nafasi ya 12 ikifundishwa na makocha watatu tofauti ambao wote walishindwa kuiokoa timu kwenye janga la kutoshiriki michuano ya Ulaya kwa msimu ujao.
Vilevile Chelsea ambayo itakuwa chini ya kocha mpya Mauricio Pochettino, itakuwa inatafuta ushindi wa kwanza kwenye uwanja wao wa nyumbani dhidi ya Liverpool ikiwa imeambulia patupu kwenye mechi tano za EPL ilizocheza na majogoo hawa.
Liverpool pia itakuwa inataka kurudi kwenye nafasi nne za juu baada ya kushindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao kutokana na kufanya vibaya kwa msimu uliopiuta.
Mbali ya mechi hii kubwa, mabingwa watetezi Manchester City wataanza harakati za kutetea taji la ligi kwa kucheza dhidi ya Burnley, mechi ambayo itamkutanisha mwanafunzi na lejendi wa Manchester City Vincent Kompany dhidi ya mwalimu wake Pep Guardiola.
Burnley ndio waliokuwa mabingwa wa Ligi Daraja la kwanza nchini England na huu ndio utakuwa mchezo wa kwanza wa ligi ukitarajiwa kucheza Ijumaa ya Agosti 11, katika uwanja wa nyumbani wa Burnley Turf Moor saa 4:00 usiku.
Mbali ya Man City, mchezo mwingine ni ule wa Arsenal ambayo msimu uliopita ilimaliza nafasi yapili yenyewe itakuwa ugenini kuumana na Nottingham Forest.
Watu wengi wanasubiri kuona ikiwa Arsenal ambayo kwa msimu uliopita ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa ikiwa itaendeleza kiwango ilichoonyesha.
Newcastle United ambayo ilimaliza kwenye nafasi yanne katika msimu uliopita yenyewe itaanza harakati zao dhidi ya vijana wa Unai Emery's Aston Villa.
Brighton itakuwa inaikaribisha Luton Town ambayo imepanda daraja wakati Everton ikiikaribisha Fulham kwenye uwanja wao wa nyumbani Goodison Park.
Sheffield United itakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani Bramall Lane kuikaribisha Crystal Palace ambayo hadi sasa bado inatafuta kocha mkuu.
Mashabiki wa Manchester United watatakiwa kusubiri hadi Jumatatu ya Agosti 14, kuishuhudia timu yao ikifungua msimu kwenye dimba la Old Trafford itakapovaana na Wolves.
Spurs itawafuata majirani zao Brentford kwenye mchezo wao wa kwanza ambao utakuwa wa kutaka kuonyesha ubabe kwani msimu uliopita ilishindwa kupata ushindi kwenye mechi zote mbili za ligi dhidi yao.
Dabi ya kwanza ya msimu inatarajiwa kupigwa Septemba 26, ambapo washika mitutu Arsenal watavaana na Tottenham katika dimba la Fly Emirates na mchezo wao wa marudiano utakuwa ni April 27, pale Tottenham Hotspur Stadium.
Kwa upande wa dabi ya Jiji la Liverpool ambayo inahusisha Everton na Liverpool mchezo wa kwanza utapigwa Oktoba 21, katika dimba la Anfield na marudiano utakuwa Machi 16 pale Goodison Park.
Manchester United na Manchester City zitakutana kwa mara ya kwanza Oktoba 28, Old Trafford kisha Machi 03 zitarudiana pale Etihad Machi 03.
Siku ya mwisho ya msimu itashuhudiwa Arsenal, Brentford, Brighton, Burnley na Chelsea zikizikaribisha Everton, Newcastle, Manchester United, Nottingham Forest na Bournemouth.
Vilevile Crystal Palace, Liverpool, Luton Town, Manchester City na Sheffield United zitafunga ligi na Aston Villa, Wolves, Fulham West Ham na Spurs.
Ratiba kamili ya msimu mzima utaipata ukurasa wa 17.