Rashford asherehekea ubingwa wa La Liga na mpenzi wake
Muktasari:
- Ubingwa huo ulishuhudiwa na Lucia pamoja na mama mzazi wa mchezaji huyo, Melanie, waliokuwepo uwanjani Camp Nou.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa England, Marcus Rashford, amesherehekea kutwaa taji lake la kwanza la ligi kuu akiwa na mpenzi wake, Lucia Loi, baada ya kuiongoza Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28, anayecheza Barcelona kwa mkopo akitokea Manchester United, alifunga bao la kwanza kwa mkwaju wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja na kuisaidia timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao Real Madrid katika mchezo wa El Clasico uliopigwa jana Jumapili, Mei, 10, 2026.
Ubingwa huo ulishuhudiwa na Lucia pamoja na mama mzazi wa mchezaji huyo, Melanie, waliokuwepo uwanjani Camp Nou.
Lucia Loi alitumia ukurasa wake wa Instagram kusambaza matukio ya furaha kutoka uwanjani, akianza na video za unyanyuaji wa kombe na fataki zilizorushwa kusherehekea ubingwa huo.
Baadaye, alitupia picha ya mfano wa kombe dogo la La Liga pamoja na picha ya pamoja (selfie) akiwa na Rashford iliyosindikizwa na ujumbe uliosema: 'Forever proud” (Najivunia wewe milele).
Wawili hao walioanza uhusiano wao tangu wakiwa shule huko Manchester, walirudiana mwaka jana baada ya kupitia vipindi kadhaa vya kuachana na kurudiana, ikiwemo kuvunjika kwa uchumba wao Juni 2023.
Msimu huu wa kwanza nchini Hispania umekuwa wa mafanikio makubwa kwa Rashford, ambapo amefanikiwa kufunga mabao 14 na kutoa pasi za mabao (asisti) 14 katika mashindano yote akiwa na jezi ya Blaugrana.
Kutokana na kiwango hicho cha kuridhisha, Barcelona sasa inayo fursa ya kumsajili Rashford kwa mkataba wa kudumu msimu ujao wa majira ya joto kwa ada ya pauni milioni 26.
Ikiwa Barcelona haitatumia kipengele hicho cha kumnunua jumla, mustakabali wa Rashford utakuwa shakani kwani Manchester United haina mpango wa kumrejesha kikosini.
Hali hii inatokana na mzozo uliotokea msimu uliopita kati yake na klabu hiyo chini ya kocha wa zamani, Ruben Amorim, hatua iliyopelekea kutolewa kwa mkopo kwenda Hispania ambako sasa amefanikiwa kufufua makali yake na kuonja ladha ya ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza.