PSG, Chelsea sasa macho kodo kwa Vinicius Jr.
Muktasari:
- Kumekuwa na ripoti kadhaa zinaoeleza kwamba Vinicius ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2027, amewekewa ofa kubwa sana na matajiri wa Saudi Arabia ambayo itakuwa ngumu kuikataa.
CHELSEA na Paris St-Germain zote zinatamani kumsajili staa wa Real Madrid, Vinicius Jr ambaye wawakilishi wake watakutana na mabosi wa Madrid kwa ajili ya kujadili hatma yake.
Kumekuwa na ripoti kadhaa zinaoeleza kwamba Vinicius ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2027, amewekewa ofa kubwa sana na matajiri wa Saudi Arabia ambayo itakuwa ngumu kuikataa.
Timu ya Saudi Arabia inayodaiwa kutaka kumsajili staa huyu ni Al-Hilal ambayo inatafuta mbadala wa Neymar ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Al-Hilal inaamini ikimsajili Vinicius atakuwa na mchango mkubwa katika timu tofauti na ilivyo sasa kwa Neymar ambaye muda mwingi huwa nje ya uwanja kutokana na majeraha.
Awali, wababe hawa walijaribu kumsajili Kylian Mbappe lakini ilishindikana baada ya fundi huyo kukataa hata kufanya nao mazungumzo.
Katika mkataba wa Vinicus kuna kipengele ambacho kinamruhusu kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Euro 1 bilioni.
Wakati huo huo Brentford imeziambia timu zinazohitaji huduma ya mshambuliaji wao raia wa Cameroon, Bryan Mbeumo ikiwemo Newcastle United kuwa staa huyo anauzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 50 milioni.
Mbeumo mwenye umri wa miaka 25, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026. Msimu uliopita alicheza mechi 11 za michuano yote na kufunga mabao manane.
ARSENAL inataka kumsajili winga wa West Ham na Ghana, Mohammed Kudus, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuziba pengo la mshambuliaji wao Leandro Trossard ambaye anawindwa na matajiri wa Saudi Arabia.
Ripoti zinaeleza West Ham inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 90 milioni ili kumuuza fundi huyo ambaye msimu huu amecheza mechi 10 za michuano yote na kufunga mabao mawili.
MABOSI wa Paris St-Germain wapo tayari kumruhusu mshambuliaji wao Randal Kolo Muani kuondoka kwa mkopo wa nusu msimu katika dirisha lijalo la majira ya baridi lakini kutakuwapo pia na kipengele ambacho kitairuhusu timu husika kumnunua jumla ikiwa itaridhishwa naye.
Timu kadhaa za Ligi Kuu England zimeonyesha nia ya kumsajili raia huyu wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 25.
BARCELONA bado inawasiliana kwa karibu na wawakilishi wa Rafael Leao katika harakati za kutaka kujua utayari wa staa huyo wa AC Milan juu ya kujiunga nao katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani.
Mambo hayajawa mazuri kwa Leao tangu kuanza kwa msimu huu ambapo amecheza mechi 12 za michuano yote. Mkataba wa fundi huyu unamalizika mwaka 2028.
SANTOS ya Brazil ipo katika mazungumzo na wawakilishi wa Neymar kwa ajili ya kumsajili staa huyo mwisho wa msimu huu baada ya mkataba wake na Al-Hilal kumalizika.
Mabosi wa Santos wana matumaini makubwa ya kumsajili fundi huyu kwa sababu ndio timu iliyomlea na aliichezea kabla ya kujiunga na Barcelona mwaka 2013.
LAZIO inataka kumsajili winga wa Rayo Vallecano na Colombia, James Rodriguez katika dirisha lijalo baada ya kuona kuna uwezekano mkubwa wa kumpata kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Vallecano.
Mkataba wa James unamalizika Juni mwakani na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 13 za michuano yote.
REAL Madrid imepanga kupigana vita dhidi ya Arsenal na Chelsea kwa ajili ya kumsajili beki wa Palmeiras na Brazil, Vitor Reis ambaye inataka kumsajili katika dirisha la majira ya baridi mwakani.
Reis ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Palmeiras na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.