Pochettino atoa maagizo mazito Chelsea

LONDON, ENGLAND. KAANZA kazi. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mauricio Pochettino kukutana na wakurugenzi wa ufundi wa Chelsea, Laurence Stewart na Paul Winstanley kujadili nini kifanyike kuelekea msimu ujao.

Poche ambaye anasubiri kutangazwa kama kocha mpya wa miamba hiyo ya Darajani kuanzia msimu ujao, inaelezwa atasaidiwa na Jesus Perez na benchi lake lote la ufundi ambalo amekuwa akihama nalo popote atakapokwenda.
Kwenye kikao hicho, mengi yamejadiliwa na kikubwa ni maeneo ya kuboresha pamoja na aina ya wachezaji watakaosajili dirisha lijalo ili kuifanya timu hiyo kurusisha makali yake baada ya kuchemka msimu huu.

Moja ya maeneo ambayo The Blue imepania kuweka nguvu ni kwenye usajili na inataka kumchukua straika wa Inter Milan na Argentina, Lautaro Martinez baada ya kuona itakuwa ngumu kumpata straika wa Napoli, Victor Osimhen, huku pia ikimuwinda kiungo wa West Ham United, Declan Rice ambaye pia anawaniwa na Arsenal, lakini bado Pochettino hajaidhinisha usajili wake.

Kwenye kikao hicho, jina la kipa wa Aston Villa, Emiliano Martinez limependekezwa kati ya makipa wengine waliotajwa.
Pia Pochettino anatamani kuona kiungo, Mason Mount anasalia kwenye timu na amepanga kumzungumza naye ili kumshawishi mara baada ya msimu kumalizika, sawa na Romelu Lukaku anayekipiga kwa mkopo Inter Milan.

Inaelezwa, Pochetino amekuwa akikutana na wakurugenzi hao mara kwa mara lengo likiwa ni kuifanya irejeshe makali yake ikiwa msimu huu ikiwa ndio mbovu zaidi tangu mwaka 1994.
Chelsea imempa uhuru Pochettino wa kusimamia shughuli zote za timu kuanzia upande wa vijana hadi wakubwa na kuijenga timu kidogo kidogo ili iwe bora zaidi kwa muda mrefu na sio mpango wa muda mfupi.

Mabosi wa Chelsea pia wamemhakikishia Pochettino atakuwa na haki ya kuamua nini kifanyike na nini kisifanyike kwenye timu ili kuepusha migongano kama ilivyokuwa hapo awali kipindi cha Thomas Tuchel hata ikasababisha kocha huyo kukosana na mmiliki Toddy Boehly.

Inaelezwa Chelsea ilitaka kumwajiri Pochettino kwa muda mrefu hata kabla ya Graham Potter lakini walisita kwa sababu umiliki ndio ulikuwa mchanga na aliwahi kuifundisha Tottenham hivyo waliona itakuwa tabu kidogo ukizingatia timu hizi mbili zimekuwa na upinzani mkali sana.

Pochettino ni miongoni mwa makocha waliowahi kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu England alipokuwa anaifundisha Tottenham kabla hajatimkia zake PSG ingawa hakuchukua taji.
Akiwa na Spurs aliiwezesha kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya kufungwa na Liverpool.

Chelsea kwa sasa inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na alama 43 baada ya kucheza mechi 35, ikishinda 11, sare 10 na kufungwa 14.