Partey, Odegaard mbona freshi

Tuesday February 23 2021
part pic

LONDON, ENGLAND. KIUNGO wa Arsenal na timu ya taifa ya Ghana, Thomas Partey amesema anafuraha kucheza sambamba na Martin Odegaard katika eneo la kiungo jambo ambalo linampa mzuka.
Odegaard, 22, raia wa Norway alisajiliwa Arsenal mwezi Januari akitokea Real Madrid kwa mkopo wa mwaka mmoja baada ya kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Madrid.
Licha ya Odegaard kutocheza mechi nyingi za kubainisha kiwango chake akiwa wababe hao lakini Partey, 27, amesema ni faida kubwa kuwa naye kwenye timu na amekubali mavitu ya kiungo huyo akikumbuka jinsi alivyokuwa akipata wakati mgumu anapokabiliana naye kwenye mechi za La Liga wakati Odegaard akiwa Real Sociedad kwa mkopo na yeye akiwa Atletico Madrid.
“Ni ngumu sana kucheza dhidi yake. Nakumbuka kucheza dhidi yake ni mjanja sana mara zote ni mwepesi akiwa na mpira hakupi nafasi ya kuupata. Inafurahisha kuwa naye hapa, naimani atakuwa na msimu mzuri na atatusaidia kufanikisha kile tunataka.”  Partey aliiambia Stadium Astro.
Odegaard alijiunga na Real Madrid mwaka 2015 akitokea klabu ya Stromsgodset akiwa na umri wa miaka 16 akionekana kama moja ya makinda chipukizi wenye kipaji kikubwa cha kucheza mpira katika ulimwengu wa soka.
Lakini mambo hayakwenda sawa huko Madrid kwani hakupata nafasi ya kucheza hali iliyosababisha atolewe kwa mkopo kwenda Heerenveen, Vitesse na Real Sociedad kisha Arsenal kwa mkopo.


Advertisement