P Diddy tajiri anayeishi kwa wasiwasi mjini

LOS ANGELES, MAREKANI. HABARI inayoenea kila kukicha kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari ni kumhusu mmoja wa malejendari wa muziki wa Hip Hop Marekani na duniani, Sean Comb Diddy maarufu kwa jina la P Diddy.

P Diddy amekuwa akitafutwa na polisi kwa tuhuma za unyanyasaji wa kingono na hivi karibuni nyumba zake zimefanyiwa upekuzi kama sehemu ya uchunguzi wa madai hayo.

Kwa sasa wasiwasi umetanda kwake kama itathibitika ni kweli ingawa bado uchunguzi unaendelea na sakata lake limekuwa gumzo kila kona.

Hata hivyo, pamoja na tuhuma hizo, anatajwa ni rapa namba mbili kwa utajiri baada ya Jay Z. Pesa si za kitoto ingawa mwisho wake unaweza usiwe mzuri kutokana na tuhuma hizo nzito, lakini hivi ndivyo anavyoishi mjini.


ANAVYOPIGA PESA

Muziki ndio chanzo chake kikuu cha kuingiza pesa na  mwaka 2022 pekee alikadiriwa kuingiza takriban Dola 50 milion zaidi ya Sh100 bilioni.

Pia ana kampuni yake ya kudizaini na kutengeneza nguo iitwayo ‘Sean John’ aliyoianzisha mwaka 1998. Diddy pia ndio bosi wa kampuni ya Combs Enterprises, inayojihusisha na uwekezaji kwenye biashara mbalimbali, pia ana hisa kwenye kampuni ya vinywaji ya Ciroc vodka na televisheni ya Revolt TV.

Akishirikiana na wafanyabiashara mbalimbali aliwahi kuinunua kampuni ya Aquahydrate na mwaka 2019 alikuwa ndiye mwekezaji mkuu wa kampuni ya PlayVS.

Amewahi kuigiza katika filamu mbalimbal kama Made (2001), A Raisin in the Sun (2008), Get Him to the Greek (2010), Draft Day (2014) na The Defiant Ones (2017), na inakadiriwa alipata zaidi ya Dola 20 milioni katika muvi zote.

Hadi kufikia mwaka 2023, kwa mujibu wa tovuti mbalimbali msanii huyu wa Hip Hop alikuwa na utajiri unaofikia Dola 1 bilioni ambao unamfanya kuwa msanii tajiri zaidi wa kiume kwenye Hip Hop baada ya Jay Z.


NDINGA

Rolls-Royce Phantom

Rolls-Royce Phantom Drophead Coupe

Lamborghini Gallardo Spyder

Ferrari 360 Spider

Ferrari F430

Chevrolet Corvette

Jeep Wrangler Unlimited

Mercedes-Maybach 57

Cadillac Escalade


MSAADA KWA JAMII

Mwaka 2003 alianzisha mbio zilizochangia zaidi ya Dola 2 milioni zilikwenda kutumika kusaidia shule na watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Amekuwa akifanya kazi na taasisi mbalimbali zinazosaidia jamii kwenye matatizpo mbalimbali, kama vile watu wanaoishi na kansa, Ukimwi na walemavu.

Katika taasisi hizo, Diddy anakadiriwa kutoa misaada ya zaidi ya Dola 5 milioni kila mwaka.


MJENGO

Septemba 2014, Diddy alilipa Dola 39 milioni kwa ajili ya kununua nyumba iliyokuwa kwenye eneo la ukubwa kilomita za mraba 17,000, Holmby Hills, huko Los Angeles.

Jumba hilo la kifahari lina bwawa la kuogelea, sehemu ya kutazamia sinema yenye viti 35, chumba cha mvuke, chumba cha masaji, saluni na chumba cha kunywea viwanyaji mbalimbali.

Pia mwaka 2009 alilipa Dola 5.25 milioni kwa ajili ya kununua nyumba ya aliyekuwa mzazi mwenzake, marehemu Kim Porter, aliyefariki mwaka 2018.

Aliiuza nyumba hiyo mwaka 2022 kwa Dola 6.5 milioni.

Vile vile mwaka 2021, msanii huyu alitoa Dola 35 milioni kwa ajili ya kununua nyumba kwenye kisiwa cha Miami inayopatikana kwenye eneo la ukubwa wa ekari 1.3.


BATA NA MAISHA BINAFSI

Hadi sasa ana watoto saba na mtoto wake wa kwanza alimpata mwaka 1993 na mwanamama Misa Hylton-Brim, akapata watoto wengine wawili wa kike na mmoja wa kiume aliozaa na Kimberly Porter aliyekuwa naye kwenye mahusiano kuanzia mwaka 1994 na 2007. Pia alipata mtoto mmoja na Sarah Chapman, mwaka 2007 aliingia kwenye mahusiano na Cassie Ventura walioachana mwaka 2018.

Mtoto wake wa sana alimpata Oktoba 2022 na alizaa na Dana Tran.