Osimhen, Gyokeres mezani Man United
Muktasari:
- Miamba hiyo ya Old Trafford inaamini itasajili mshambuliaji mpya kwenye dirisha lijalo, jambo ambalo litamfanya Marcus Rashford, anayecheza Aston Villa kwa mkopo kwa sasa ataondoka jumla.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imeripotiwa kupewa ripoti kila wiki ya kuhusu hali ya mastraika Victor Osimhen na Viktor Gyokeres endapo kama watapatikana sokoni kwenye dirisha lijalo la usajili.
Miamba hiyo ya Old Trafford inaamini itasajili mshambuliaji mpya kwenye dirisha lijalo, jambo ambalo litamfanya Marcus Rashford, anayecheza Aston Villa kwa mkopo kwa sasa ataondoka jumla.
Man United imekuwa ikivutiwa na washambuliaji Osimhen na Gyokeres kwa muda mrefu, huku wakali hao wakicheza kwenye vikosi vya Galatasaray na Sporting Lisbon mtawalia.
Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, Man United imekuwa ikipewa ripoti kila wiki juu ya maendeleo ya wachezaji hao, alisema kwenye kolamu yake ya Give Me Sport: "Kuna uvumi mwingi sana kuhusu Man United kuvutiwa na washambuliaji Osimhen na Viktor Gyokeres.
"Lakini, bajeti ni kitu kinachoelezwa kuwa muhimu kwenye dirisha lijalo la usajili ili kwenda sawa na sera ya usawa kwenye mapato na matumizi. Hivyo, hakuna dili iliyokamilika tayari, kinachofanyika ni kufuatilia tu.
"Man United imetuma skauti wake kufuatia maendeleo ya Osimhen huko Galatasaray. Imekuwa ikifanya hivyo pia kwa Gyokeres."
Straika wa Kinigeria, Osimhen amekuwa kwenye kiwango bora tangu alipojiunga na Galatasaray, ambako tayari ameshafunga mabao 20 msimu huu na kuasisti mara tano. Gyokeres, naye mambo yake ni moto, akifunga mabao 35 na asisti nane katika mechi 37 alizocheza msimu huu.