Onana atumika kumshawishi Mbeumo

Muktasari:
- Mbeumo amekuwa akisakwa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kuwa na msimu bora huko Brentford. Alikuwa staa wa klabu hiyo akifunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu England na sasa anajiandaa kwenda kujiunga na timu kubwa.
LONDON, ENGLAND: KIPA wa Manchester United, Andre Onana ameripotiwa kutumia muda wake mwingi kumshawishi mchezaji mwenzake wa Cameroon, Bryan Mbeumo kujiunga na chama hilo linalonolewa na Ruben Amorim baada ya sasa vita ya kuwania saini yake kuwa kali kutokana na Tottenham Hotspur nayo kumtaka.
Mbeumo amekuwa akisakwa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kuwa na msimu bora huko Brentford. Alikuwa staa wa klabu hiyo akifunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu England na sasa anajiandaa kwenda kujiunga na timu kubwa.
Man United imekuwa moja ya timu inayotaka saini yake, lakini baada ya kocha Thomas Frank kujiunga na Spurs, jambo hilo limefanya Mbeumo kuwa kwenye sakata kali la kuchagua aende wapi kwenye pande hizo mbili.
Mbeumo anafahamu wazi anahitajika kwa nguvu zote huko Old Trafford, ambako kocha Amorim anajaribu kukifuma upya kikosi chake baada ya kumaliza vibaya msimu uliopita, ikishika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi, huku ikiwa tayari imeshamnyakua Matheus Cunha.
Ripoti zinafichua kwamba Onana anafanya kila analoliweza kumshawishi Mbeumo kuichagua Man United mbele ya Tottenham, ambapo wawili hao wamekuwa na uhusiano mzuri wakiwa kwenye timu yao ya taifa ya Cameroon.
Mbeumo na Onana wamekuwa wakicheza pamoja kwenye timu ya taifa, ambako winga huyo wa Brentford, alianza kuchezea kikosi cha Simba Wasioshindika mwaka 2022. Mbeumo hadi sasa ameshacheza mechi 22, wakati Onana ametumikia timu hiyo kwenye mechi 48. Man United imeshawasilisha Pauni 60 milioni za kumnasa Mbeumo, lakini Brentford iliigomea, wakati Spurs inaripotiwa kupeleka ofa ya Pauni 70 milioni, huku ikiwa na silaha ya kocha Frank, kwamba anaweza kumshawishi mchezaji huyo ili wakaungane pamoja huko London.
Mbeumo alizungumza kuhusu kocha Frank na kusema: "Yeye (Frank) amenifanyia makubwa sana. Alionyesha kuniamini tangu mwanzo. Aliniongoza mimi kama binadamu na mchezaji."