Nyingine zajitokeza dili la Kobbie Mainoo
Muktasari:
- Kwa sasa Man United bado wapo katika mazungumzo na mabingwa hao watetezi wa Serie A kuhusu uhamisho wa mkopo wa mshambuliaji Rasmus Hojlund, ambao itahusishwa kipengele cha kumnunua mazima.
MANCHESTER, ENGLAND: LICHA ya uwepo wa vigogo, Real Madrid, Bayern Munich na hata Bayer Leverkusen wanaohitaji saini ya kiungo wa Manchester United, Kobbie Mainoo, Napoli pia imejitosa katika vita ya kuiwania huduma ya staa huyo.
Kwa sasa Man United bado wapo katika mazungumzo na mabingwa hao watetezi wa Serie A kuhusu uhamisho wa mkopo wa mshambuliaji Rasmus Hojlund, ambao itahusishwa kipengele cha kumnunua mazima.
Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, Napoli pia imeulizia uwezekano wa kuipata huduma ya Mainoo katika majadiliano yaliyoanza mapema wiki hii.
Napoli ambayo tayari ina Scott McTominay, ikiwa itafanikisha kumpata Hojlund na McTominay itakuwa imesajili wachezaji watatu kutoka Man United katika kipindi cha miezi 12.
Mabosi wa Napoli wanamshawishi Mainoo kujiunga nao kwa ahadi ya kumpa fursa ya kucheza mara kwa mara katika kikosi pia kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jambo ambalo halipati kwa sasa Man United.
Fursa ya kucheza Ligi ya Mabingwa pia kumeipa Napoli nafasi zaidi mbele ya majirani zao Roma ambao pia wanahitaji huduma yake.
Hata hivyo, Napoli haipewi nafasi kubwa sana kwa sababu tayari kuna vigogo wakubwa wametu mezani kutaka huduma ya kiungo huyo na ofa ambazo zinaaminika kuwa bora zaidi ya ile ambayo Napoli inataka kuitoa.
Licha ya Napoli kumpa ahadi ya kucheza mara kwa mara, lakini katika eneo la kiungo anatarajiwa kukutana na ushindani wa kutoha kuanzia kwa McTominay ambaye ni mchezaji bora wa Serie A msimu uliopita, pia katika dirisha hili amesajiliwa Kevin De Bruyne wakati huo huo katika timu kuna viungo wengine kama Frank Anguissa na Stanislav pamoja na Billy Gilmour ambaye hapati nafasi ya kutosha.
Mainoo amekuwa na wakati mgumu kwa kutopata nafasi ya kucheza chini ya Ruben Amorim ambapo tangu msimu huu uanze hajacheza hata dakika moja. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.