Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Noti zamwagika Man United

Muktasari:

  • Klabu hiyo sasa imeingia kwenye faida ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kuchangiwa na kupunguza wafanyakazi takribani 45, kukatwa na kufutwa kwa bonasi za wafanyakazi.

MANCHESTER, ENGLAND: HATUA kali za kupunguza gharama za matumizi zilizoanzishwa na tajiri wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe zimezaa matunda makubwa na kuzalisha faida katika kikosi cha mashetani wekundu.

Klabu hiyo sasa imeingia kwenye faida ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kuchangiwa na kupunguza wafanyakazi takribani 45, kukatwa na kufutwa kwa bonasi za wafanyakazi.

Kwenye hesabu za klabu, Man United imepata faida ya uendeshaji ya Pauni 32.6 milioni katika miezi sita ya kwanza ya mwaka wa fedha, ikilinganishwa na hasara ya Pauni 3.9 milioni katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Vyanzo vya Man United vinasema klabu hiyo inaanza kuona matokeo chanya ya kifedha ya mageuzi ya nje ya uwanja tangu uwekezaji wa Ratcliffe ulipofanyika Februari 2024.

Bilionea huyo wa kampuni ya Ineos alidhamiria kufanya mageuzi makubwa baada ya kununua hisa na kuikuta klabu hiyo ikiwa na deni la Pauni 1.1 bilioni.

Ratcliffe, 73, amepunguza gharama katika sekta mbalimbali kwenye klabu hiyo, ikiwamo kufuta sherehe ya Krismasi ya kila mwaka na kumuondoa Sir Alex Ferguson kwenye nafasi yake ya kulipwa kama balozi wa klabu.

Alipandisha pia bei za tiketi hadi Pauni 66 na kupunguza mzigo wa mishahara, mambo ambayo yote yamechangia kupatikana kwa faida hiyo.

Bila ya mapato ya uwanjani na fedha za haki za matangazo ya Ulaya, faida za Man United zimeongezeka kwa Pauni 40 milioni ikilinganishwa na miezi sita iliyotangulia.

Ripoti hiyo ya kifedha ambayo ilitolewa Jumatano, inaonyesha mapato ya viingilio vya uwanjani yamepungua kwa Pauni 2.5 milioni kutoka Pauni 52 milioni hadi Pauni 49.5 milioni kutokana na timu kushiriki  mashindano machache.

Mapato ya kibiashara pia yameshuka kwa Pauni 6 milioni hadi Pauni 78.55 milioni, lakini mapato ya matangazo yameongezeka kidogo kwa Pauni 0.7 milioni hadi kufikia Pauni 62.3 milioni.

Kwa sasa Man United haina mdhamini wa jezi za mazoezi tangu mkataba wao na Tezos ulipomalizika msimu uliopita, na udhamini wa AON uliisha mwaka 2021.

Mapato ya jumla yameshuka kutoka Pauni 198.7 milioni 198.7 hadi Pauni 190.3 milioni hususani baada ya kushindwa kufuzu kucheza michuano ya Ulaya msimu huu.