Neves aingia kwenye moto wa mashabiki wa Ronaldo, apoteza wafuasi milioni 2
Muktasari:
- Neves amekuwa gumzo mitandaoni tangu baada ya sare ya 1-1 iliyoipata Ureno dhidi ya DR Congo katika mchezo wa kwanza wa kundi K la michuano ya Kombe la Dunia 2026, ambapo alidaiwa kueleza kuwa Ronaldo ni mchezaji wa kawaida kama wengine.
MIAMI, MAREKANI: KIUNGO wa Ureno na klabu ya PSG, Joao Neves, amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuripotiwa kupoteza zaidi ya wafuasi milioni mbili kwenye mtandao wa Instagram kufuatia kauli yake dhidi ya nahodha wa timu hiyo, Cristiano Ronaldo.
Neves amekuwa gumzo mitandaoni tangu baada ya sare ya 1-1 iliyoipata Ureno dhidi ya DR Congo katika mchezo wa kwanza wa kundi K la michuano ya Kombe la Dunia 2026, ambapo alidaiwa kueleza kuwa Ronaldo ni mchezaji wa kawaida kama wengine.
Kauli hiyo iliwakasirisha baadhi ya mashabiki wa Ronaldo duniani ambao waamini kwamba nahodha huyo hakupewa heshima anayostahili kutokana na mafanikio yake makubwa katika soka duniani.
Mara baada ya mahojiano hayo kusambaa, akaunti za Neves kwenye mitandao ya kijamii zilianza kushambuliwa kwa maoni mazito kutoka kwa mashabiki wa Ronaldo, huku ripoti mbalimbali za mtandaoni zikidai kuwa kiungo huyo alipoteza zaidi ya wafuasi milioni mbili ndani ya muda mfupi.
Inadaiwa kabla ya mechi hiyo Neves alikuwa na wafuasi milioni tano, lakini baada ya kumzungumzia Ronaldo walipungua hadi hii leo, Juni 20, 2026 kubakia milioni tatu.
Mbali na kupungua kwa idadi ya wafuasi, sehemu ya maoni kwenye picha zake za Instagram ilifurika ujumbe kutoka kwa mashabiki waliokuwa wakimtetea Ronaldo na kumshutumu Neves kwa kile walichodai ni kukosa heshima kwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka.
Mambo yalikuwa magumu zaidi baada ya ujumbe wa kughushi uliodaiwa kutoka kwa mpenzi wa Neves kusambaa kwa kasi mitandaoni uliodaiwa kuwa jibu kwa shabiki aliyependekeza Neves ampasie Ronaldo mpira mara nyingi zaidi akiwa uwanjani yaani "Pass to Ronaldo."
Ingawa baadaye ilielezwa kuwa haukuwa wa kweli, tayari ulikuwa umeongeza hasira za mashabiki na kuzidisha shinikizo kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21.
Sakata hilo limeibua mjadala mkubwa ndani na nje ya Ureno kuhusu kauli za wachezaji kwa mashabiki, hasa linapohusishwa jina la Ronaldo ambaye bado anaungwa mkono kwa nguvu na maelfu ya mashabiki duniani licha ya kuwa katika hatua za mwisho za kumalizia maisha yake ya soka.