Ndiaye wa USM Alger ni kocha wa mataji
Muktasari:
- Kocha Ndiaye mwenye uzoefu mkubwa anakuwa kocha wa tano katika historia ya soka la Afrika kushinda mashindano yote mawili makubwa ya klabu ya CAF lile la Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya USM Alger kuifunga Zamalek SC kwa mikwaju ya penalti 8-7 katika fainali ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Cairo International.
Dakar, Senegal: Kocha wa Msenegali, Lamine Ndiaye aingia katika historia ya soka la Afrika baada ya kuiongoza USM Alger kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha Ndiaye mwenye uzoefu mkubwa anakuwa kocha wa tano katika historia ya soka la Afrika kushinda mashindano yote mawili makubwa ya klabu ya CAF lile la Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya USM Alger kuifunga Zamalek SC kwa mikwaju ya penalti 8-7 katika fainali ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Cairo International.
Kwa Ndiaye, ushindi huu ulikuwa zaidi ya kuongeza kombe jingine.
Ulikuwa ni sura mpya katika safari yake ndefu ya ukocha barani Afrika, iliyodumu kwa miongo kadhaa na kujaa mataji, mafanikio ya kuibua timu upya, na usiku wa kihistoria kuanzia Afrika Kaskazini hadi Afrika ya Kati.
Akiwa na umri wa miaka 69, Ndiaye bado ni mmoja wa makocha wanaoheshimika zaidi Afrika — ingawa ni mtu wa utulivu na asiyejitangaza sana. Uwezo wake wa kuongoza kwa utulivu na mbinu zake za kiufundi vimemletea mafanikio mara kwa mara kwenye majukwaa ya soka.
USM Alger ilitwaa ubingwa huo baada ya kuhimili presha kutoka kwa Zamalek mbele ya maelfu ya mashabiki walioujaza Uwanja wa Cairo.
Timu ya Misri ilishinda mchezo wa marudiano kwa 1-0 kupitia penalti ya mapema ya Oday Al-Dabbagh, na kufanya matokeo ya jumla kuwa 1-1, kufuatia ushindi wa USM Alger katika mchezo wa kwanza huko Algiers.
Ushindi huo pia uliihakikishia USM Alger kitita cha rekodi cha dola milioni 4 za Marekani, kufuatia ongezeko la zawadi za mashindano ya klabu lililotangazwa na CAF hivi karibuni.
Hata hivyo, baada ya fainali hiyo macho mengi yalielekezwa kwa mtu aliyesimama kwa utulivu pembeni mwa uwanja — Lamine Ndiaye.
Mafanikio haya yanamweka katika kundi maalum la makocha waliofanikiwa kushinda mashindano yote mawili makubwa ya klabu Afrika.
Orodha hiyo ya kipekee inawajumuisha kocha Mtunisia, Faouzi Benzarti, gwiji wa Ghana, Cecil Jones Attuquayefio, kocha wa Mmorocco Houcine Ammouta, na Mtunisia Moine Chaabani.
Sasa Ndiaye ameungana nao baada ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa CAF akiwa na TP Mazembe mwaka 2010, na sasa ametwaa Kombe la Shirikisho akiwa na USM Alger mwaka 2026.
Mafanikio haya yanaonyesha uimara wa kocha ambaye ametumia miongo mingi kujijenga na thibitisha ubora wake katika klabu anazofundisha Afrika.
Ndiaye alianza kujulikana zaidi kimataifa wakati alipokuwa na mafanikio akiwa na TP Mazembe, alipoiongoza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa msimu wa 2009–10 na kuifanya klabu hiyo ya Lubumbashi kutawala soka Afrika.
Baadaye alizinoa timu mbalimbali ikiwemo Coton Sport FC de Garoua, Horoya AC, na Al Hilal Omdurman, ambapo aliendelea kushinda mataji ya ndani na kufanya vizuri kimataifa.
Kinachoendelea kumtofautisha ni uwezo wake wa kuhimili presha katika mechi kubwa zaidi Afrika.
Dhidi ya Zamalek, USM Alger ilionyesha nidhamu na utulivu ambao umekuwa alama ya timu zake.
Kwa Ndiaye, filimbi ya mwisho ilithibitisha rasmi hadhi yake kama mmoja wa wabobezi wa kudumu wa soka la Afrika.
Katika kipindi ambacho soka linazidi kutawaliwa na makocha vijana na mbinu mpya za kisasa, kocha huyu mkongwe wa Senegal ameendelea kuthibitisha kuwa uzoefu, utulivu na uelewa wa kina wa soka la Afrika bado vina thamani kubwa.
Baada ya usiku mwingine wa kihistoria jijini Cairo, jina la Ndiaye sasa limeandikwa miongoni mwa magwiji wa makocha wa soka katika klabu barani Afrika.