Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamuzi wa kike Mmarekani kuandika rekodi Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo itakayopigwa Alhamisi, Juni 18, 2026, kwenye Uwanja wa Atlanta, Marekani, inamfanya Penso kuandika rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Marekani kuchezesha mechi ya Kombe la Dunia la wanaume.

ATLANTA, MAREKANI: MWAMUZI wa kike kutoka Marekani, Tori Penso anatarajiwa kuandika rekodi baada ya leo Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kumteua kusimamia mechi ya pili ya kundi A Kombe la Dunia kati ya Afrika Kusini dhidi ya Jamhuri ya Czech.

Katika mechi hiyo itakayopigwa Alhamisi, Juni 18, 2026, kwenye Uwanja wa Atlanta, Marekani, inamfanya Penso kuandika rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Marekani kuchezesha mechi ya Kombe la Dunia la wanaume.

Afrika Kusini inayowakilisha  Afrika inatafuta ushindi wa kwanza katika fainali za Kombe la Dunia, baada ya mechi ya kwanza kuchapwa mabao 2-0 na Mexico sawa na Jamhuri ya Czech iliyochapwa na Korea Kusini 2-1.

Penso atakuwa mwanamke wa kwanza kutoka Marekani kuchezesha mechi ya Kombe la Dunia la wanaume, akiungana na wanawake wengine waliochezesha 2022 Qatar ambao ni Stephanie Frappart wa Ufaransa na Yoshimi Yamashita wa Japan.

Mwamuzi mwingine wa kike aliyeweka rekodi hiyo 2022 huko Qatar ni Salima Mukansanga wa Rwanda, ambapo Penso amefuata nyayo za waamuzi wengine wa kike.


TORI PENSO NI NANI?

Mwamuzi huyo jina lake kamili ni Mary Victoria Penso ambaye amezaliwa Julai 8, 1986, Stuart, Florida Marekani, ambapo alianza kazi ya uamuzi 2015 katika Ligi ya Wanawake ya Marekani (NWSL).

Mwaka 2019, Penso alihamia Ligi Daraja la Pili la Wanaume  Marekani (USL), na tangu 2020 amekuwa mwamuzi Kwenye Ligi Kuu Marekani (MLS), huku mumewe Chris Penso ni mwamuzi wa muda mrefu wa MLS.

Januari 2020, Penso aliteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa Chama Cha Maofisa wa Soka wa Vyuo Vikuu Marekani, akiwa ni mwamuzi pia wa FIFA tangu 2021.

Penso alikuwa  miongoni mwa sehemu ya waamuzi wa Kombe la Dunia la Wanawake 2023  lililofanyika Australia na New Zealand, ambapo alipangiwa kuchezesha fainali ya Kombe la Dunia, akiwa ni mwamuzi wa kwanza kutoka Marekani.

Pia, Penso alihudumu kwenye Kombe la Dunia la Klabu lililofanyika Marekani 2025, akichezesha mechi ya ufunguzi kati ya Juventus inayoshiriki Ligi Kuu Italia iliyocheza na Al Ain FC ya Falme ya Kiarabu (UAE).

Mwamuzi huyo aliendelea kung'ara katika michuano hiyo  baada ya kuchezesha pia mechi ya hatua ya makundi kati ya Borussia Dortmund ya Ujerumani dhidi ya Ulsan HD ya Korea Kusini.

Kazi nyingine ya Penso anayofanya ni utaalamu wa masoko ya kidijitali akihusika kukuza bidhaa na kusimamia matangazo ya mtandaoni kwenye majukwaa tofauti kama Facebook, Instagram, Google na TikTok.

Penso ni miongoni mwa waamuzi nane kutoka Marekani walioteuliwa na FIFA kuchezesha Kombe la Dunia 2026 akiungana na Ismail Elfath, Brooke Mayo, Kyle Atkins, Kathryn Nesbitt, Corey Parker, Joe Dickerson pamoja na Armando Villarreal.