Mwamuzi Japan, Tunisia kuvaa jezi maalumu
Muktasari:
- Mechi hiyo ya Kundi F itakayochezwa saa moja asubuhi kesho, mjini Guadalupe huko Monterrey, Mexxico, itakuwa ya 1,000 katika historia ya Kombe la Dunia la wanaume.
MONTERREY, MEXICO: MWAMUZI wa Romania, Istvan Kovacs, atavaa jezi maalumu atakapochezesha mchezo wa Kombe la Dunia kati ya Japan dhidi ya Tunisia.
Mechi hiyo ya Kundi F itakayochezwa saa moja asubuhi kesho, mjini Guadalupe huko Monterrey, Mexxico, itakuwa ya 1,000 katika historia ya Kombe la Dunia la wanaume.
Katika kuadhimisha tukio hilo la kihistoria, Kovacs atavaa jezi ya waamuzi yenye mapambo pamoja na beji ya dhahabu iliyoandikwa “1000”.
Katika video maalumu, mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya FIFA na mwamuzi wa zamani, Pierluigi Collina, amemkabidhi Kovacs jezi hiyo na kuelezea umuhimu wake.
Collina amesema: “Mechi ya 1,000 ni Japan dhidi ya Tunisia. Ni mechi maalumu sana katika historia ya Kombe la Dunia. Fikiria kuwa mwamuzi wa mchezo huu wa kipekee. Unastahili kitu maalumu, ndiyo maana kuna dhahabu kwenye mistari na beji ya namba 1000.”
Kombe la Dunia limekuwapo kwa miaka 96 tangu mashindano ya kwanza ambayo Uruguay ilibeba ubingwa 1930, na sasa ni moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo duniani.
Japan inaingia katika mchezo huo baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Uholanzi. Hata hivyo, Japan imekumbwa na majeraha kwa wachezaji muhimu ambapo Kaoru Mitoma alitolewa kabla ya mashindano, Wataru Endo aliumia na baadaye kustaafu soka la kimataifa huku
Takefusa Kubo akiumia goti na kuondoka uwanjani akiwa kwenye kiti cha magurudumu.
Kwa upande wa Tunisia tayari imefanya mabadiliko ya kocha baada ya kupoteza kwa baoa 5-1 dhidi ya Sweden.
Kocha huyo wa awali, Sabri Lamouchi, aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na gwiji wa soka la Afrika, Herve Renard, ambaye ana uzoefu mkubwa katika Kombe la Dunia na michuano ya Afcon aliyepewa mkataba wa hadi mwisho wa mashindano hayo.