Munoz atua Anfield, sasa wafukuzia Diomande
Muktasari:
- Liverpool wamethibitisha usajili wa Munoz kutoka CA Osasuna baada ya kuamsha kipengele chake cha kuachiliwa cha euro40 milioni.
LONDON, England: LIVERPOOL wamekamilisha usajili wa winga wa Hispania, Victor Munoz, huku pia wakiijulisha RB Leipzig kuwa wako tayari kutoa euro100 milioni kwa ajili ya winga Yan Diomande.
Liverpool wamethibitisha usajili wa Munoz kutoka CA Osasuna baada ya kuamsha kipengele chake cha kuachiliwa cha euro40 milioni.
Munoz ni sehemu ya kikosi cha Hispania katika Kombe la Dunia, huku Liverpool wakituma maafisa wao nchini Marekani kufanikisha vipimo vya afya vya mchezaji huyo Jumatano.
Diomande pia yuko kwenye Kombe la Dunia akiwa na Ivory Coast. Ingawa Paris Saint-Germain pia wanamuhitaji, bado hawajawasilisha ofa rasmi, jambo linaloiweka Liverpool katika nafasi nzuri ya kumsajili kijana huyo mwenye umri wa miaka 19.
Hata hivyo, Leipzig wanataka zaidi ya kiwango ambacho Liverpool wako tayari kulipa, na pia hawana nia ya kumuachia mchezaji huyo katika dirisha hili la usajili.
Kuna uelewa kwamba ikiwa Diomande atafanya vizuri katika Kombe la Dunia, thamani yake inaweza kuongezeka zaidi. Inaripotiwa kuwa ofa inayozidi euro130 milioni inaweza kubadilisha msimamo wa Leipzig.
Diomande alifunga mabao 12 na kutoa pasi nane za mabao katika msimu uliopita wa Bundesliga.
Munoz asaini mkataba wa miaka sita
Munoz mwenye umri wa miaka 22, ambaye alicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa mwezi Machi, ana uwezo wa kucheza pande zote mbili za ushambuliaji na anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka sita katika Uwanja wa Anfield.
Liverpool watalipa ada hiyo kwa awamu mbili.
Newcastle United walikuwa wamefika hatua nzuri katika mazungumzo ya kumsajili baada ya kumuuza Anthony Gordon kwenda FC Barcelona, lakini Liverpool wamefanikiwa kushinda mbio hizo.
Msimu uliopita Munoz alifunga mabao saba na kutoa pasi tano za mabao katika mechi 36.
Atakuwa usajili wa kwanza wa Liverpool tangu kuwasili kwa kocha mpya Andoni Iraola, aliyerithi nafasi ya Arne Slot mapema mwezi huu.
Kutoka La Masia hadi Anfield
Munoz ni zao la akademi maarufu ya FC Barcelona ya La Masia kabla ya kuhamia Real Madrid, ambako alicheza mechi mbili kama mchezaji wa akiba katika La Liga.
Baadaye alijiunga na Osasuna mwezi Julai 2025 kwa euro milioni tano.
Madrid walikuwa na haki ya kupata asilimia 50 ya faida ya mauzo yake ya baadaye pamoja na haki ya ulinganisha ofa yoyote iliyowasilishwa kwa mchezaji huyo.
Klabu hiyo ilifikiria kumrudisha, lakini wasiwasi kuhusu muda wa kucheza chini ya kocha Jose Mourinho ulifanya mpango huo usiendelee.
Barcelona pia walionyesha nia ya kumsajili kabla ya kukamilisha usajili wa Anthony Gordon kwa zaidi ya pauni69 milioni.
Liverpool wamekuwa wakifanikiwa kuwashinda Newcastle katika usajili wa wachezaji muhimu, kama ilivyotokea kwa Hugo Ekitike na baadaye Alexander Isak.
Kwa nini Iraola anamtaka Munoz?
Munoz anacheza zaidi upande wa kushoto licha ya kutumia mguu wa kulia. Kasi yake, uwezo wa kuvunja safu za ulinzi zilizojipanga nyuma na ubora wake katika eneo la mwisho la ushambuliaji ni miongoni mwa sababu zilizomfanya Iraola asisitize usajili wake.
Liverpool wanaamini bado ana nafasi kubwa ya kuimarisha takwimu zake za mabao na pasi za mabao, jambo linaloonekana kwenye mkataba wa muda mrefu wa miaka sita waliompa.
Pia wanaamini kuwa kuwasili kwake hakutapunguza muda wa kucheza kwa Ngumoha mwenye miaka 17, ambaye alicheza mechi yake ya kwanza kwa England mwezi huu.
Wakati huo huo, kuna maslahi kutoka Italia kwa mshambuliaji wa Liverpool Federico Chiesa, ambaye anataka kupata muda zaidi wa kucheza baada ya kuanza mechi moja tu ya Ligi Kuu msimu uliopita.