Mshindi tuzo ya Ballon d'Or anavuta mkwanja kiasi gani?
Muktasari:
- Katika kipengele cha wanaume kwa tuzo hiyo ya Ballon d’Or, wanaopewa nafasi kubwa ni Ousmane Dembele wa PSG pamoja na washambuliaji wa Barcelona, Lamine Yamal na Raphinha, lakini anayepewa nafasi kubwa zaidi ni Dembele.
PARIS, UFARANSA: Sherehe za Ballon d’Or mwaka 2025 zinatarajiwa kufanyika leo kuanzia saa 4:00 usiku katika ukumbi wa Theatre du Chatelet, Paris, Ufaransa na ulimwengu wa soka unasubiri kwa hamu kuwaona washindi wa vipengele mbalimbali kwa upande wa wanaume na wanawake.
Katika kipengele cha wanaume kwa tuzo hiyo ya Ballon d’Or, wanaopewa nafasi kubwa ni Ousmane Dembele wa PSG pamoja na washambuliaji wa Barcelona, Lamine Yamal na Raphinha, lakini anayepewa nafasi kubwa zaidi ni Dembele.
Ballon d’Or ya mwaka 2025 pia itakuwa na kipengele cha mchezaji bora kinda wakike ambapo mchezaji maarufu wa Colombia, Linda Caicedo kutoka Madrid anaonekana kuwa na asilimia nyingi za kuchukua. Pia tuzo zitatolewa kwa kocha bora na klabu bora ya msimu.
Wakati wengi wakidhani tuzo ya Ballon d’Or inajumuisha zawadi kubwa ya fedha, ukweli ni tofauti, hakuna malipo ya moja kwa moja ya kifedha.
Tuzo hiyo inayoandaliwa Shirikisho la Soka Ufaransa na lile Ulaya (UEFA), inajumuisha kikombe cha Ballon d’Or ambacho kinakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 3,500, ingawa hakitengenezwi kwa dhahabu moja kwa moja.
Licha ya kutokuwa na zawadi ya fedha, lakini faida ya kushinda Ballon d’Or ni kubwa. Klabu mara nyingi hutoa bonasi na motisha kwa wachezaji wanaotajwa, na kampuni nyingi huingia mikataba ya ubalozi wa mamilioni ya pesa kwa wachezaji wanaoshinda tuzo hizo.