Msako wa kocha Burkina Faso, Steve McClaren achomoza
Muktasari:
- Taifa hilo la Afrika Magharibi, liko mbioni kumteua kocha mkuu mpya kabla ya mapumziko ya kimataifa ya mwezi Machi mwaka huu, kufuatia kufutwa kazi kwa Brama Traoré baada ya Burkina Faso kutolewa hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON 2025 iliyofanyika Morocco.
ALIYEKUWA kocha wa timu ya taifa ya England na klabu kadhaa za Ligi Kuu nchini humo, Steve McClaren, ameripotiwa kuingia katika orodha ya mwisho ya wagombea wa nafasi ya kuifundisha Burkina Faso.
Taifa hilo la Afrika Magharibi, liko mbioni kumteua kocha mkuu mpya kabla ya mapumziko ya kimataifa ya mwezi Machi mwaka huu, kufuatia kufutwa kazi kwa Brama Traoré baada ya Burkina Faso kutolewa hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON 2025 iliyofanyika Morocco.
Kwa mujibu wa taarifa, Shirikisho la Soka la Burkina Faso (FBF), lilipokea takribani maombi 100 ya makocha waliowania nafasi hiyo. Miongoni mwa waliotuma maombi hayo ni pamoja na aliyewahi kuinoa Kaizer Chiefs, Giovanni Solinas.
Hata hivyo, sasa orodha hiyo imepunguzwa hadi chini ya wagombea kumi, huku McClaren akiwa miongoni mwao. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 64, hana timu ya kufundisha tangu alipojiuzulu kama kocha wa timu ya taifa ya Jamaica, Novemba 2025.
McClaren anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kocha wa Stade Malien, Mauril Njoya, ambaye hivi karibuni aliiongoza klabu hiyo kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambako watakutana na Mamelodi Sundowns.
Majina mengine yanayoripotiwa kuwa kwenye orodha ya mwisho ni Kamou Malo, Amir Abdou, Pascal Dupraz, Antonio Conceicao da Silva Oliveira, Vahid Halilhodzic na Vincenzo Alberto Annese.
Uamuzi wa mwisho unatarajiwa kutolewa hivi karibuni huku mashabiki wa Burkina Faso wakisubiri kwa hamu kujua nani atakayekabidhiwa jukumu la kuiongoza timu hiyo katika kampeni zijazo za kimataifa.