Mourinho anapiga tu pesa kijanja
Muktasari:
- Mourinho, 62, amekuwa akikusanya fidia za kufutwa kazi na sasa akiweka mkwanja mrefu mfukoni baada ya kufunguliwa mlango wa kutokea huko Fenerbahce baada ya kushindwa kuipa tiketi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya timu hiyo kufutia kupoteza mbele ya Benfica katika mechi ya mchujo.
ISTANBUL, UTURUKI: JOSE Mourinho ameweka mfukoni mkwanja mrefu karibu Pauni 100 milioni kwa sababu moja tu ya kufutwa kazi kwenye timu anazozinoa.
Mourinho, 62, amekuwa akikusanya fidia za kufutwa kazi na sasa akiweka mkwanja mrefu mfukoni baada ya kufunguliwa mlango wa kutokea huko Fenerbahce baada ya kushindwa kuipa tiketi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya timu hiyo kufutia kupoteza mbele ya Benfica katika mechi ya mchujo.
Mourinho alijiunga na klabu hiyo ya Istanbul mwaka 2024 ikiwa ni miezi sita tangu alipofutwa kazi AS Roma. Na licha ya kumaliza msimu mikono mitupu Fenerbahce, hiyo ni timu ya pili kwa Mourinho kushindwa kubeba taji lolote baada ya Tottenham, lakini fidia yake anayolipwa kwa mkataba wake kuvunjwa ni pesa nzuri.
Ripoti zinafichua kwamba Mourinho atalipwa fidia ya Pauni 13 milioni na klabu hiyo ya Uturuki baada ya mkataba wake kuvunjwa. Jambo hilo linamfanya Mourinho makusanyo yake yote ya pesa alizolipwa baada ya mikataba yake kuvunjwa kufikia Pauni 100 milioni.
Mourinho alilipwa Pauni 26.3 milioni alipofutwa kazi Chelsea katika awamu mbili tofauti, wakati huko Manchester United alilipwa Pauni 19.6 milioni alipoonyeshwa mlango wa kutokea.
Aliwahi kuinoa Real Madrid pia na ilipomfuta kazi ilimlipa fidia ya Pauni 17 milioni, huko Tottenham Hotspur ilipochoshwa na huduma yake na kuamua kuachana naye, ilimlipa Pauni 15 milioni. AS Roma ndiyo timu iliyomlipa fidia ndogo Mourinho, Pauni 3 milioni.
Kwa kujumlisha Pauni 13 milioni ya fidia atakayolipwa na klabu hiyo ya Uturuki, Mourinho sas amekusanya kiasi cha Pauni 93 milioni kutokana na kupoteza kazi.