Mo Salah azua gumzo
Muktasari:
- Salah ambaye alifunga bao la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu England wikiendi iliyopita dhidi ya Brighton kwenye dimba la Anfield, mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu na anahusishwa kutimkia Saudi Arabia.
LIVERPOOL, ENGLAND: STAA wa Liverpool, Mohamed Salah amezua utata juu ya hatma yake kwenye timu hiyo baada ya ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.
Salah ambaye alifunga bao la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu England wikiendi iliyopita dhidi ya Brighton kwenye dimba la Anfield, mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu na anahusishwa kutimkia Saudi Arabia.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo walioshinda mabao 2-1, Salah aliweka picha yake katika mitandao ya kijamii kisha akaandika: "Tupo kileleni, mahali ambapo timu hii inapaswa kuwa, hakuna cha ziada, kila timu huwa inashinda mechi lakini mwisho wa yote, bingwa ni mmoja na hicho ndicho tunachokihitaji, asanteni sana kwa sapoti yenu usiku wa jana, vyovyote vile itakavyokuwa, sitosahau hisia za kufunga bao kwenye Uwanja wa Anfield zilivyo."
Ujumbe huo uliibua maswali mengi na mashabiki wengi walichukua kauli yake aliyosema 'Vyovyote itakavyokuwa' ndio iliyoibua mjadala ikionekana kuwa ana hatihati ya kubaki Anfield.
Tangu ajiunge na Liverpool mwaka 2017, Salah amefunga mabao 220 katika mechi 364 za michuano yote.
Pia ameshinda taji la Ligi Kuu England mara moja, Ligi ya Mabingwa Ulaya moja sawa na FA Cup, pia ameshinda Carabao mara mbili.
Hadi kufikia sasa, bado kuna maswali mengi juu ya hatma ya mastaa wa Liverpool wanaomaliza mikataba yao mwisho wa msimu huu ikiwa pamoja na Trent Alexander-Arnold na Virgil van Dijk ambao hadi sasa hawajafikia nao mwafaka wa kuwaongeza.