Mo Salah aipa ubingwa Arsenal
Muktasari:
- Msimu uliopita, Salah na wachezaji wenzake wa Liverpool walibeba taji la Ligi Kuu huku Arsenal ikimaliza nafasi ya pili kwa mara ya tatu mfululizo.
LIVERPOOL, ENGLAND: STAA wa Liverpool, Mohamed Salah anaamini Arsenal inaweza kuwa kwenye nafasi bora zaidi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, baada ya miaka mitatu ya kuambulia patupu licha ya kuwa kwa muda mrefu katika mbio za ubingwa.
Msimu uliopita, Salah na wachezaji wenzake wa Liverpool walibeba taji la Ligi Kuu huku Arsenal ikimaliza nafasi ya pili kwa mara ya tatu mfululizo.
Klabu hiyo ya Kaskazini mwa London mara ya mwisho ilitwaa ubingwa wa ligi miaka 20 iliyopita, msimu wa 2003/04, na sasa iko kwenye shauku kubwa ya kukomesha ukame huo wa muda mrefu.
Kabla ya kuanza msimu huu, Liverpool ilionekana ndiyo inapigiwa upatu zaidi kutetea ubingwa wake baada ya kufanya usajili mkubwa na kuimarisha kikosi cha kocha Arne Slot.
Hata hivyo, pamoja na Liverpool kuanza vyema kampeni yao kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya Bournemouth Ijumaa usiku, Salah anakiri kuwa ubora wa kikosi cha Arsenal ambacho kimekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitano kinawafanya kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa zaidi za kushinda taji.
Akihojiwa kuhusu nafasi ya Arsenal kwenye tuzo za PFA usiku wa Jumanne, Salah alisema: “Nadhani wana kikosi kizuri sana msimu huu kama mlivyokuwa msimu uliopita. Kwa hiyo wana nafasi nzuri kweli. Nadhani wao ndiyo wanaopigiwa upatu kwa sasa kwa sababu mchezaji waowengi wamekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitano. Siwezi kusema nitawatakia kila la kheri kwa sababu nina imani sisi ndio tutachukua ubingwa tena.”
Maoni ya Salah kuhusu Arsenal yanafanana na ya mchambuzi wa Sky Sports, Gary Neville, ambaye mapema wiki hii alisema ni vigumu kutabiri nani ataibuka bingwa kati ya Arsenal, Liverpool na Manchester City. Hata hivyo, aliongeza kuwa Arsenal imekuwa na kiwango bora kwa miaka mitatu mfululizo na anaamini mwaka huu unaweza kuwa wakwao.