Mkongwe wa soka Gabon auawa
Muktasari:
- Taarifa za vyombo vya habari vya Gabon na Ufaransa zinadai mwili wa Musavu-King ulipatikana nyuma ya nyumba moja mjini Libreville, huku ripoti zikieleza kuwa mazingira ya kifo chake bado hayajulikani na uchunguzi unaendelea.
LIBREVILLE, GABON: MWANASOKA wa zamani wa kimataifa wa Gabon, Yrondu Musavu-King, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 34 katika mazingira ambayo yameacha fumbo kuhusiana na kifo chake.
Taarifa za vyombo vya habari vya Gabon na Ufaransa zinadai mwili wa Musavu-King ulipatikana nyuma ya nyumba moja mjini Libreville, huku ripoti zikieleza kuwa mazingira ya kifo chake bado hayajulikani na uchunguzi unaendelea.
Musavu-King alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Gabon, ambapo alicheza mechi 12 za kimataifa na kuiwakilisha katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Katika maisha yake ya soka alichezea klabu kadhaa Ulaya, hususan Ufaransa na mongoni mwazo ni Toulouse, Lorient, Caen na Le Mans. Pia aliwahi kucheza nje ya Ufaransa katika klabu za Granada (Hispania), Udinese (Italia) na St. Gallen nchini Uswisi.
Mchezaji huyo alistaafu soka 2022 baada ya kucheza msimu mmoja Bengaluru FC nchini India, ikiwa ni klabu yake ya kwanza nje ya Ulaya.
Caen ambako alianza soka na baadaye kucheza timu ya wakubwa, ilituma ujumbe kwa familia na marafiki wa marehemu ikiwatakia faraja, huku Le Mans ikieleza kushtushwa na taarifa hizo ikikumbuka mchango wa beki huyo ambaye aliichezea 2019 katika Ligi Daraja la Pili Ufaransa.
Kwa upande mwingine, Udinese ya Italia pia ilitoa salamu za rambirambi zake.
Kifo cha Musavu-King kimeacha simanzi katika familia ya soka Gabon na Ulaya, huku mashabiki, wachezaji wa zamani na klabu mbalimbali wakituma salamu za pole kufuatia kuondokewa na mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa.