Mkhitaryan afichua Mourinho alivyomfanya aondoke Man United
Muktasari:
- Licha ya kwamba alikuwa mmoja wa wachezaji wa mwanzo mwanzo kabisa waliosajiliwa na Mourinho baada ya kutua Old Trafford, lakini kocha huyo Mreno hakuonekana kumpa thamani ya juu winga huyo wa mpira.
MILAN, ITALIA: KIUNGO Henrikh Mkhitaryan amefichua ugomvi wake na kocha Jose Mourinho na ndio chanzo kilichomfanya afikie mwisho wa zama zake kuitumikia Manchester United.
Staa huyo wa Armenia mwenye umri wa miaka 36, aliichezea Man United kati ya 2016 na 2018.
Licha ya kwamba alikuwa mmoja wa wachezaji wa mwanzo mwanzo kabisa waliosajiliwa na Mourinho baada ya kutua Old Trafford, lakini kocha huyo Mreno hakuonekana kumpa thamani ya juu winga huyo wa mpira.
Mkhitaryan alihama Old Trafford baada ya miezi 18 tu ya kujiunga na Man United, alitimkia zake Arsenal katika dili lililomhusisha mshambuliaji Alexis Sanchez, akihamia upande mwingine.
Katika kitabu chake kimya, kilichochapishwa huko Italia, staa huyo wa Inter Milan, Mkhitaryan alibainisha mambo yalivyokuwa kwenye miezi yake ya mwisho huko Man United.
Aliandika kuhusu Mourinho: “Nilimwambia, umekuwa ukinikosoa sana kwa karibu mwaka na nusu sasa, tangu nilipowasili Manchester United.
“Mourinho aliniambia, nilikuwa hovyo, hilo lilinikasirisha. ‘Nilimjibu ni wewe ndo wa hovyo. Hovyo kabisa.’
“Mourinho alijibu: ‘Ondoka, sitaki kukuona tena.’
“Katika kipindi cha mazoezi, kocha alikuwa haniongeleshi kitu, alikuwa kimya tu, lakini kila ilipofika jioni, alikuwa akitumia meseji kwenye WhatsApp. ‘Miki, ondoka, tafadhali.’
“Hiyo hali ilikuwa mbaya sana. Nilikuwa nikimjibu mara zote kwa meseji ileile niliyokuwa nimemjibu awali, hivyo ilikuwa ni copy na paste. Nitaondoka nikipata timu sahihi, la nitaendelea kubaki hapa hadi mwisho wa msimu.
“Katikati ya Januari, meseji zilianza kubadilika. Alituma ‘Miki, ondoka tafadhali, hiyo ndiyo njia nitakayoweza kumpata Alexis Sanchez.’
“Mino Raiola alikuwa akifanya huu usajili wa kubadilishana wachezaji na Arsenal. Jibu langu lilikuwa mbaya kiasi, nilimjibu ‘Siondoki kwa sababu nikusaidie kupata unachotaka, tafadhali acha kunitumia meseji. Kama unataka, zungumza na Mino.’”
Mkhitaryan kisha alimaliza kwa kuandika: “Na baada ya hapo kila mtu akaisha kwa furaha.”
Sanchez, ambaye pia umri wake wa sasa ni miaka 36, alikwenda kuwa na wakati mgumu huko Old Trafford.
Staa huyo wa Chile alifunga mabao matano tu katika mechi 45 alizoichezea Man United, alishindwa kabisa kufanya maajabu licha ya kulipwa mshahara, uliokaribia Pauni 450,000 kwa wiki.
Mkhitaryan naye hakuwa na maajabu huko kwenye kikosi cha Arsenal alikohamia, ambapo kipindi hicho ilikuwa chini ya kocha Arsene Wenger, ambapo alicheza mechi 59, huku timu yake ya Arsenal ilimaliza nafasi ya tano katika msimu wa 2018-19.
Aliondoka Arsenal kwenda kujiunga na AS Roma, ambapo awali uhamisho huo ulikuwa wa mkopo, Septemba 2019.
Kilichofurahisha ni kwamba alikwenda kukutana tena na Mourinho kwenye kikosi hicho cha AS Roma baada ya kocha huyo Mreno kutua Stadio Olimpico mwaka 2021.
Wawili hao awali walioneka na kama wasingemaliza tofauti zai baada ya Mourinho kusema mwaka 2022: “Kitu kinachonifurahisha ni kwamba huko mwanzoni watu walikuwa wakichukulia kinyume, walipojaribu kusema ‘Mkhitaryan na Jose hawawezi kufanya kazi, Jose ni aina ya mtu ambaye ukitibuana naye, basi mambo hayawezi kuwa vizuri tena’.
“Mambo yamekuwa kinyume chake, sisi ni watu tuliopevuka na tumekuwa wa kweli kwa kila mtu.”
Mourinho aliongeza: “Nina furaha kwa ajili yake na nimefurahi kwamba watu wameanza kunialewa kwamba mimi si mtu wa nyeusi ni nyeusi na nyeupe ni nyeupe.”
Mkhitaryan aliondoka AS Roma na kwenda kujiunga na Inter Milan kwa uhamisho wa bure mwaka uliofuatia kitu ambacho kiliripotiwa kumwaacha kocha Mourinho akiwa na hasira.
Staa huyo anayeweza kucheza winga ya kushoto au kulia pamoja na Namba 10, ameitumikia Inter Milan mara 154 na panga pangua amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya Serie A.
Na kinachovutia zaidi, baada ya kufika San Siro, alipata nafasi ya kucheza timu moja na Alexis Sanchez, mtu ambaye awali walipishana getini wakati anaingia Arsenal na mwenzake anakwenda upande wa pili kwa maana ya Man United. Wawili hao walicheza pamoja Inter msimu wa 2023-24.