Milan walivyomtimua Massimiliano Allegri
Muktasari:
- Milan walimaliza nafasi ya tano katika Ligi Kuu Italia (Serie A) na kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Allegri alihitimisha msimu kwa kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Cagliari, Jumapili iliyopita, huku kikosi chake kikishinda mechi moja kati ya nne za mwisho.
MILAN, ITALIA: AC Milan wamemfuta kazi kocha Massimiliano Allegri baada ya kumaliza msimu vibaya, huku uongozi wa klabu ukiutaja kama kushindwa kulikotokana na namna benchi la ufundi lilivyokuwa likitekeleza mipango yake.
Milan walimaliza nafasi ya tano katika Ligi Kuu Italia (Serie A) na kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Allegri alihitimisha msimu kwa kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Cagliari, Jumapili iliyopita, huku kikosi chake kikishinda mechi moja kati ya nne za mwisho.
Katika taarifa yake, Milan ilisema: “Mwisho wa msimu ulikuwa tofauti kabisa na kiwango tulichoonyesha hapo awali. Kipigo kimeufanya msimu huu kuwa tulioshindwa bila kupinga.”
Allegri alirudi San Siro msimu huu kwa kipindi chake cha pili baada ya kuinoa klabu hiyo kati ya 2010 na Januari 2014.
Taarifa mbalimbali zinamhusisha kocha wa zamani wa Bournemouth, Andoni Iraola, kwamba anaweza kukabidhiwa kazi hiyo.
Iraola aliiongoza Bournemouth kufuzu Europa League kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 127 ya klabu hiyo, baada ya Bournemouth kumaliza nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu England na sasa wataingia msimu mpya chini ya kocha mpya, Marco Rose.
Iraola pia aliwahi kuhusishwa na kazi ya ukocha Manchester United kabla klabu hiyo kuamua kubaki na Michael Carrick kutokana na matokeo mazuri aliyopata katika nusu ya pili ya msimu.
Mafanikio ya Iraola yalikuwa makubwa zaidi kutokana na kupoteza wachezaji muhimu wakiwamo Dean Huijsen aliyekwenda Real Madrid, Milos Kerkez (Liverpool) na Ilya Zabarnyi (PSG).