Mikah afuta ubingwa Man City kisa Rodri
Muktasari:
- Mshindi huyo wa Ballon D’Or alikuwa nje ya uwanja sehemu kubwa ya msimu uliopita baada ya kuumia goti Septemba mwaka jana. Na sasa kiungo huyo alipata maumivu ya misuli ya korodani wakati wa fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani na hivyo atakuwa nje ya uwanja hadi Oktoba.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa zamani wa Manchester City, Micah Richards ameifuta timu hiyo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kwasababu kiungo Rodri atakuwa nje ya uwanja hadi Oktoba.
Mshindi huyo wa Ballon D’Or alikuwa nje ya uwanja sehemu kubwa ya msimu uliopita baada ya kuumia goti Septemba mwaka jana. Na sasa kiungo huyo alipata maumivu ya misuli ya korodani wakati wa fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani na hivyo atakuwa nje ya uwanja hadi Oktoba.
Man City ilifanya usajili mkubwa kwenye dirisha la Januari na kusajili tena kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kumaliza msimu bila taji.
Lakini, beki wa zamani wa Man City, Richards anaamini Rodri, ambaye alisajiliwa kwa Pauni 62 milioni mwaka 2019 bado mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola.
“Kama Rodri angekuwa fiti, nadhani wangekuwa moto, lakini hayupo fiti hadi pengine Oktoba huko,” alisema mchambuzi huyo wa Sky Sports.
“Nadhani hilo linabadili mengi kuwahusu wao, kwa sababu yeye ni muhimu katika ishu ya kuzuia mashambulizi ya kushtukiza.
“Tijjani Reijnders aliyesajiliwa kutoka Milan ni mchezaji mzuri, anaweza kucheza Namba 6, Namba 8 na anafunga pia, kama alivyofanya kwenye mechi za pre-season. Lakini, ukiangalia kwenye eneo hilo la katikati ya uwanja, mfano msimu uliopita, kijana Nico Gonzalez, hakuonekana kuwa na uwezo kwenye Namba 6, alionekana zaidi kuwa ni Namba 8.
“Rayan Cherki naye anaweza kuwa mchezaji muhimu, lakini kwenye Namba 10, anaweza kucheza kulia, kushoto, hodari kwenye miguu yote,
“Kwenye ubingwa, Liverpool watakuwapo, ambao wanapewa nafasi kubwa msimu huu. Nadhani kuna Chelsea pia wanakuja vizuri kama tulivyowaona kwenye Kombe la Dunia la Klabu. Na tumekuwa tukizungumza Arsenal kwa muda kwamba inahitaji straika, na sasa imemsajili.”