Messi aacha utata Argentina, akisaidia ushindi wa 3-0
Muktasari:
- Messi ambaye katika mchezo huo alipachika mabao mawili huku lingine likifungwa na Lautaro Martinez amesema kuwa hafikirii kama atakuwa na muda mrefu wa kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo.
Lionel Messi usiku wa kuamkia leo ameiongoza Argentina kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Venezuela lakini baada ya hapo akatoa kauli inayoonekana kama ni ya kuwaaga kwa mara ya mwisho mashabiki ndani ya ardhi ya kwao.
Messi ambaye katika mchezo huo alipachika mabao mawili huku lingine likifungwa na Lautaro Martinez amesema kuwa hafikirii kama atakuwa na muda mrefu wa kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo.
Baada ya mchezo huo, Argentina haitocheza tena mechi ya kimashindano katika ardhi ya kwao hadi Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakapomalizika huko Marekani, Canada na Mexico jambo ambalo linamfanya Messi ajione kama analazimika kuwaaga mashabiki wa nyumbani.
"Kama nilivyosema hapo nyuma kuhusu Kombe la Dunia kwamba sidhani kama nitacheza tena. Kwa sababu ya umri wangu, kitu kinachoingia zaidi akilini ni sitoweza kucheza.
"Ninajitahidi kujisikia vizuri na zaidi ya yote kuwa mkweli kwangu. Pale ninapojisikia vizuri ninafurahi lakini nisipojisikia, sina muda mzuri hivyo nachagua kutokuwepo kule kama sitojisikia vizuri. Sijafanya uamuzi bado kuhusu Kombe la Dunia," amesema Messi.
Messi amesema kuwa bado anao muda wa kutosha kujitathmini na kufanya uamuzi kama ataitumikia Argentina katika Kombe la Dunia lijalo au hatofanya hivyo.