Mbeumo kupewa jezi anayoipenda
Muktasari:
- Man United bado ipo kwenye mazungumzo ya klabu ya Brentford, lakini mambo yanashindwa kufikia tamati kwa zaidi ya mwezi sasa kutokana na Brentford kuhitaji pesa nyingi kwa mchezaji huyo, ambaye ilimsajili kwa Pauni 5.8 milioni mwaka 2019.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA, Bryan Mbeumo anatarajia kwenda kukabidhiwa jezi Namba 19 atakapojiunga na Manchester United, kutokana na namba huyo kuwa wazi huko Old Trafford.
Man United bado ipo kwenye mazungumzo ya klabu ya Brentford, lakini mambo yanashindwa kufikia tamati kwa zaidi ya mwezi sasa kutokana na Brentford kuhitaji pesa nyingi kwa mchezaji huyo, ambaye ilimsajili kwa Pauni 5.8 milioni mwaka 2019.
Kulikuwa na ugumu wa makubaliano ya pande mbili, lakini kinachoelezwa kwa sasa, Man United imepeleka ofa ya tatu ya Pauni 70 milioni, ikiamini hiyo itatosha kuwashawishi Brentford kumuuza staa wao huyo.
Mbeumo yupo tayari kwa uhamisho wa kwenda Old Trafford na kama hilo likifanikiwa staa huyo atakwenda kuongeza kipato chake pia kutokana na kukabidhiwa dili tamu.
Staa huyo mara zote amekuwa akicheza akiwa amevaa jezi Namba 19, ambapo anatumia namba hiyo kwenye klabu ya Brentford na timu ya taifa ya Cameroon.
Na kama atatua Man United, basi atakwenda kukabidhiwa jezi hiyo.
Jezi yenye namba hiyo kwa sasa ipo wazi. Mchezaji wa mwisho kuvaa jezi Namba 19 kwenye kikosi cha Man United alikuwa beki wa kati, Raphael Varane, ambaye aliachana na timu hiyo mwaka jana kwenda kujiunga na timu ya Como ya Serie A.
Kuhusu Mbeumo, Man United ilishuhudia ofa zao mbili zilikataliwa, ikiwamo ya Pauni 62.5 milioni - pesa ambayo ilitosha wakati ilipomsajili Matheus Cunha kutoka Wolves.
Lakini, Brentford imekomaa kuhakikisha Man United inalipa pesa zaidi ya iliyopita kwa Cunha kwa sababu Mbeumo alionyesha kiwango bora msimu uliopita kumzidi staa huyo wa Kibrazili na pia umri wake bado ni mdogo.
Mbeumo alifunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu England akiwa na Brentford msimu uliopita na amekuwa moja ya wachezaji wanaofukuziwa kwenye dirisha hili. Kwa ujumla wake, amefunga mabao 70 katika mechi 242 alizochezea Brentford mwaka 2019.