Mbeumo ajilipua Man United, awageukia wenzake
Muktasari:
- Mbeumo, aliyesajiliwa katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu kwa dau la Pauni 65 milioni, akihojiwa na Sky Sports alisema: "Nadhani kila mmoja ndani ya timu anatakiwa kuwajibika. Unapochezea klabu kubwa kama hii, unapaswa kujua nini cha kufanya, kama timu, tunapaswa kufanya vizuri zaidi."
MANCHESTER, ENGLAND: NYOTA wa Manchester United, Bryan Mbeumo, amewataka wachezaji wenzake wawajibike kufuatia mwanzo mbaya wa msimu huu.
Mbeumo, aliyesajiliwa katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu kwa dau la Pauni 65 milioni, akihojiwa na Sky Sports alisema: "Nadhani kila mmoja ndani ya timu anatakiwa kuwajibika. Unapochezea klabu kubwa kama hii, unapaswa kujua nini cha kufanya, kama timu, tunapaswa kufanya vizuri zaidi."
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon alichagua kujiunga na Man United badala ya Tottenham Hotspur ambayo ilitamani sana kumsajili.
Mambo yanaonekana kuwa magumu kwake tofauti na ilivyotarajiwa kwani Man United imepoteza mechi tatu kati ya sita za kwanza za Ligi Kuu England na kutolewa kwenye Kombe la Carabao hatua ya kwanza baada ya kuchapwa kwa penalti na Grimsby Town ya Ligi Daraja la Nne.
Katika mchezo huo, Mbeumo ndiye aliyekosa penalti ya kuamua, jambo lililosababisha kuondolewa kwao mapema.
Katika kipindi kifupi tu, Mbeumo amegundua ukubwa wa presha inayomkabili yeye na klabu kwa ujumla pale anapokuwa hajacheza vizuri.
Japokuwa hali hii si ya kawaida kwake, amesema ataendelea kuzingatia kujiboresha zaidi kiwanjani na hatasikiliza kelele za nje.
"Bila shaka hali si nzuri lakini jambo pekee tunatakiwa kulizingatia kwa sasa ni sisi wenyewe na kutosikiliza kile kinachozungumzwa nje bali ndani ya klabu."
Mbeumo anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Man United kitakachocheza Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Sunderland kwenye Uwanja wa Old Trafford.