Mbappe avaa jezi maalumu, apambana kutetea kiatu cha dhahabu Kombe la Dunia
Muktasari:
- Tofauti hiyo haikuwa katika rangi wala muundo wa jezi, bali alionekana akiwa na alama maalumu ya rangi ya dhahabu kwenye mkono wa kulia, kitu ambacho hakikuwepo kwa wachezaji wengine wa Ufaransa akiwemo mshindi wa Ballon d'Or, Ousmane Dembele.
NEW JERSEY, MAREKANI: MASHABIKI wengi waliofuatilia mchezo wa Kundi I wa Kombe la Dunia 2026 kati ya Ufaransa na Senegal walibaki na maswali baada ya kugundua kuwa nahodha wa Ufaransa, Kylian Mbappe, alikuwa amevaa jezi tofauti kidogo na wachezaji wenzake.
Tofauti hiyo haikuwa katika rangi wala muundo wa jezi, bali alionekana akiwa na alama maalumu ya rangi ya dhahabu kwenye mkono wa kulia, kitu ambacho hakikuwepo kwa wachezaji wengine wa Ufaransa akiwemo mshindi wa Ballon d'Or, Ousmane Dembele.
Alama hiyo maalumu ni ishara ya heshima anayopata mchezaji aliyeshinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu (Golden Boot) katika Kombe la Dunia.
Mbappe alipata heshima hiyo baada ya kumaliza Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar akiwa mfungaji bora wa mashindano hayo akiwa na mabao manane.
Katika fainali ya Qatar 2022, Mbappe aliandika historia kwa kufunga mabao matatu dhidi ya Argentina lakini juhudi zake hazikutosha kuipa Ufaransa ubingwa kwani walipoteza kwa mikwaju ya penalti mbele ya timu iliyoongozwa na Lionel Messi.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid alionyesha mapema kuwa bado ana kiu ya kutetea tuzo yake ya Golden Boot baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Senegal kwenye mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia leo, Jumatano Juni 17, 2026.
Bao lake la pili lilikuwa la kuvutia zaidi baada ya kupiga shuti lililomshinda kipa wa Senegal na kuwafanya mashabiki wa Ufaransa kutamba kwenye uwanja wa MetLife.
Mbappe sio mchezaji pekee anayebeba alama hiyo ya Golden Boot katika Kombe la Dunia la mwaka huu. Wapo pia nahodha wa England, Harry Kane, aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 2018 nchini Russia, pamoja na James Rodriguez wa Colombia aliyekuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Hata hivyo, historia inaonyesha kuwa kutetea Kiatu cha dhahabu sio jambo rahisi. Tangu tuzo hiyo ianzishwe, hakuna mchezaji aliyewahi kushinda Golden Boot katika Kombe la Dunia mbili mfululizo.
Aliyekaribia zaidi kufanya hivyo ni Thomas Muller wa Ujerumani. Muller alishinda Golden Boot mwaka 2010 kwa mabao matano, kisha akamaliza nafasi ya pili mwaka 2014 baada ya kufunga mabao matano tena.
Kwa Mbappe, mabao mawili dhidi ya Senegal hayakumsaidia tu kuanza vyema mbio za Golden Boot, bali pia yaliendelea kuimarisha nafasi yake katika vitabu vya historia vya soka la Ufaransa.
Mabao hayo yamemfikisha kwenye jumla ya mabao 58 akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Ufaransa, rekodi inayomfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa nchi hiyo baada ya kumpita Olivier Giroud.
Mbali na hilo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 sasa amefikisha mabao 14 katika historia ya Kombe la Dunia, akibakiwa na mabao mawili pekee kumfikia kinara wa muda wote wa mashindano hayo, Miroslav Klose, aliyefunga mabao 16.
Iwapo ataendelea katika kasi hii, Mbappe ana nafasi kubwa ya kuvunja rekodi hiyo kabla ya kumalizika kwa Kombe la Dunia 2026, jambo ambalo litamfanya kuingia kwenye orodha ya wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kushiriki mashindano hayo.