Mbappe aipeleka Ufaransa mtoano akimfukuzia Messi kwa mabao
Muktasari:
- Mechi hiyo ambayo ilisimama kwa zaidi ya saa moja na nusu kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na radi, ilikuwa ya ushindani wa aina yake.
Pennsylvania, Marekani: UFARANSA inaungana na Mexico, Marekani, Ujerumani na Argentina kufuzu mapema hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Iraq mabao 3-0 katika mechi ya Kundi I iliyopigwa Uwanja wa Philadelphia, Marekani.
Mechi hiyo ambayo ilisimama kwa zaidi ya saa moja na nusu kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na radi, ilikuwa ya ushindani wa aina yake.
Mvua hiyo ilianza kunyesha kabla ya kumalizika kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza ambapo hadi wachezaji wanakwenda vyumbani kwa ajili ya mapumziko, bado ilikuwa inaendelea ikiambatana na radi.
Hadi dakika 15 za mapumziko zinamalizika ili timu zirudi uwanjani, mvua bado iliendelea kunyesha na kufanya wachezaji kushindwa kurejea kuendelea kucheza kwa wakati.
Wakati hali hiyo inatokea, Ufaransa ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Kylian Mbape dakika ya 14 akimalizia pasi ya Michael Olise.
Mbappe ambaye ni nahodha wa Ufaransa, alikuwa nyota wa mechi hiyo baada ya kufunga mabao mawili. Lingine alipachika dakika ya 54 kabla ya Ousmane Dembélé kuongeza la tatu dakika ya 66 na kuifanya Les Bleus kushinda mechi zote mbili kwenye kundi hilo ikifikisha pointi sita kileleni mwa kundi I, ikiiacha Iraq mkiani bila pointi.
Mbali na Mbappe kuipeleka timu hiyo mtoano, mabao hayo mawili yamemfanya mshambuliaji huyo wa Real Madrid kufikisha 16 katika historia ya Kombe la Dunia, akilingana na mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani, Miroslav Klose aliyekuwa kinara wa muda wote wa wafungaji wa mashindano hayo.
Rekodi hiyo ya Klose imekuja kuvunjwa Juni 22, 2026 na Lionel Messi wa Argentina baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Austria iliyomfanya nyota huyo kufikisha idadi ya mabao 18.
Kwa sasa unaweza kusema vita imehamia kwa Messi na Mbappe kwani wawili hao wanafukuzana kwa mabao.
Ukiangalia orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia, Messi ana mabao 18, akimuacha mawili Mbappe.
Pia orodha ya wafungaji bora wa fainali hizo mwaka huu, Messi anaongoza akiwa na mabao matano, akifuatiwa na Mbappe mwenye manne sawa na Erling Haaland.