Maumivu ya gharama EPL!
Muktasari:
- Utafiti unaonyesha, Man United ilirekodi ama namba moja au mbili kwa klabu zilizotumia pesa nyingi kugharimia wachezaji majeruhi kati ya msimu wa 2020/21 na 2024/25.
LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United imeingia gharama kubwa kwa wachezaji majeruhi katika kipindi cha misimu mitano iliyopita ikitumia Pauni 155 milioni, ikiwa ni kiwango kikubwa kuliko klabu nyingine yoyote kwenye Ligi Kuu England.
Utafiti unaonyesha, Man United ilirekodi ama namba moja au mbili kwa klabu zilizotumia pesa nyingi kugharimia wachezaji majeruhi kati ya msimu wa 2020/21 na 2024/25.
Takwimu zilizotolewa na Howden's Men's European Football Injury Index, ripoti ambayo si tu ilizingatia zaidi msimu uliopita, wakati Man United ilipokuwa kwenye kiwango cha hovyo katika kipindi cha miaka 50, ilionyesha gharama iliyotumia timu hiyo kwa kugharimia wachezaji majeruhi kwa kipindi cha misimu mitano iliyopita.
Katika kipindi hicho, Man United sambamba na timu za Manchester City, Liverpool na Chelsea, zimekuwa na gharama kubwa kutokana na kuhudumia wachezaji majeruhi. Baada ya Man United kutumia Pauni 155 milioni, inafuatia Chelsea iliyotumia Pauni 137 milioni na Man City imetumia Pauni 104 milioni. Gharama za mchezaji majeruhi zinahesabiwa kwa mshahara wake wa siku kwa kipindi ambacho atakuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha.
Hiyo ina maana kama mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa atakuwa nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi, gharama yake inakuwa kubwa ukilinganisha na wachezaji wenye mishahara midogo.
Man United msimu wao ghali zaidi ambao walitumia pesa nyingi kulipa wachezaji majeruhi ni 2023/24, Pauni 45.28 milioni, wakati msimu uliopita, majeruhi waliwagharamia Pauni 28 milioni, kwa mujibu wa utafiti huo.
Gharama ya chini ambayo Man United ilitumia kwa wachezaji majeruhi ni Pauni 14.5 milioni katika msimu wa 2020/21, ambapo ilimaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer. Kwa kipindi cha miaka mitano, Man United imeshuhudia majeruhi 399, ikiwa ni wastani wa majeruhi 80 kwa msimu.
Chelsea ilishuhudia majeruhi 359, wakati Newcastle ilirekodi majeruhi 355. Licha ya kuwa na mambo mabaya uwanjani msimu uliopita, Man United ilirekodi visa 68 vya majeruhi, kikiwa ni kiwango cha chini kwa kipindi hicho.
Utafiti huo ulihusisha pia ligi za Ujerumani, Hispania, Italia na Ufaransa na zilirekodi majeruhi 22,596 na kugharimu karibu Pauni 3 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano. Klabu za Ligi Kuu England zinashikilia asilimia 24 ya majeruhi hayo, lakini ni zaidi ya asilimia 40 ya gharama zilizotumika kulipa wachezajai waliokuwa wagonjwa.