Mastaa Newcastle wana kitu cha Isak
Muktasari:
- Straika huyo hajasafiri na wachezaji wenzake kwenye Mashariki ya Mbali kwenye pre-season baada ya kudaiwa anapiga hesabu za kuondoka.
NEWCASTLE, ENGLAND: MASTAA wa Newcastle United, Bruno Guimaraes na Dan Burn wamefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu ishu ya Alexander Isak kutaka kuachana na miamba hiyo ya St James’ Park.
Straika huyo hajasafiri na wachezaji wenzake kwenye Mashariki ya Mbali kwenye pre-season baada ya kudaiwa anapiga hesabu za kuondoka.
Jambo hilo limezifanya timu nyingi kutaka saini yake, ikiwamo mabingwa wa Ligi Kuu England, Liverpool, huku hatima ya Isak ikiwa kwenye mashaka.
Staa huyo wa kimataifa wa Sweden, ambaye alifunga mabao 27 katika mechi 42 alizocheza msimu uliopita ni mmoja wa washambuliaji matata kabisa duniani.
Sasa beki, Burn amefichua kitu kuhusu uelewa wake juu ya hatima ya maisha ya Isak kwenye kikosi hicho cha St James’ Park.
Alisema: “Sikia, kila mtu ana maoni yake. Lakini, ninachofikiri, tunaweza kuhimili kile tunachoweza kukihimili. Hilo ni swali analopaswa kujibu Alex. Bila shaka ni mchezaji mkubwa kwetu, lakini tunaowachezaji wengine wenye vipaji wapo kwenye kikosi hiki. Tumemleta Anthony (Elanga) pia, usajili mzuri.”
Newcastle ilibainisha kukosekana kwa Isak kwenye ziara ya pre-season ya timu hiyo ni kutokana na straika huyo kuwa majeruhi na Burn, 33, aliongeza kwenye hilo:
“Alex hakufanya mazoezi kwa sababu anasumbuliwa na maumivu ya paja kwa muda sasa.”
Nahodha wa Newcastle, Guimaraes, 27, alisema: “Nipo naye karibu sana. Ni kijana mzuri. Amekuwa kwenye kipindi kigumu kwa sasa. Kipaumbele changu ni kwa wachezaji. Isak ishu yake siwezi kuihimili, ni ya klabu.
“Natumaini atakuwa fiti atakaporudi Newcastle kujiandaa na msimu mpya. Tulichoambiwa amebaki Newcastle kwa sababu ni majeruhi. Ni mchezaji mkubwa na ni pigo kutokuwapo kwenye ziara. Tunamhitaji haraka iwezekanavyo.”
Isak bado ana mkataba wa miaka mitatu na hivi karibuni aligomea dili jipya ambalo lingemfanya alipwe Pauni 300,000 kwa wiki kwenye kikosi hicho.