Mastaa nane kupigwa bei aje Gyokeres

Muktasari:
- Straika huyo wa Sporting Lisbon, Gyokeres kwa sasa yupo kwenye vita kali akigonganisha Arsenal na Manchester United zinazotaka saini yake dirisha hili la uhamisho wa kiangazi.
TURIN, ITALIA: JUVENTUS imepanga kupiga bei mastaa wanane akiwamo straika Dusan Vlahovic na kiungo Douglas Luiz ili kumudu mshahara wa mchezaji mpya inayemtaka Viktor Gyokeres.
Straika huyo wa Sporting Lisbon, Gyokeres kwa sasa yupo kwenye vita kali akigonganisha Arsenal na Manchester United zinazotaka saini yake dirisha hili la uhamisho wa kiangazi.
Lakini, Juventus inataka kutunisha misuli kuchuana kwenye dili hilo. Na kuonyesha kwamba ipo siriazi, miamba hiyo ya Italia imempa Gyokeres ofa ya mshahara wa Pauni 11 milioni kwa mwaka ili aachane na mpango wa kwenda Ligi Kuu England na badala yake akakipige Serie A. Hata hivyo, ili kufanikisha dili hilo, Juventus inahitaji kuwa na mkwanja mrefu kwa sababu ada ya mchezaji huyo ni Pauni 68.1 milioni na ziada ya Pauni 8.5 milioni zinazotakiwa na Sporting. Kwa mujibu wa Corriere dello Sport, Juventus ipo tayari kuuza wachezaji sita ili kupata pesa kukamilisha dili. Kwenye orodha hiyo yupo straika Vlahovic na kiungo wa zamani Aston Villa, Luiz, na inahitaji kuvuna walau Pauni 50 milioni. Lloyd Kelly ambaye pia amesajiliwa kutoka Newcastle dirisha hili, naye anaweza kuuzwa.
Samuel Mbangula, Daniele Rugani, Filip Kostic, Mattia Perin na Arkadiusz Milik ni mastaa wengine kwenye orodha hiyo, ambapo Juventus, imelenga walau kupata Pauni 85 milioni kwenye mauzo ya mastaa hao dirisha hili.
Wakati Juventus ikipanga kuwekeza kwa Gyokeres, miamba hiyo ina mpango mwingine ambapo inawapigia hesabu Randal Kolo Muani na Jonathan David. Wachezaji wengine kwenye rada ya Juventus ni washambuliaji Victor Osimhen na Mateo Retegui.