Mastaa Manchester City wamlilia Pep Guardiola
Muktasari:
- Guardiola, 55, alitangaza wiki iliyopita kuwa anaaondoka Man City baada ya miaka 10 ya mafanikio makubwa, ambapo ameiongoza timu hiyo kushinda mataji 20.
MANCHESTER, ENGLAND: NGULI wa mpira wa kikapu duniani, Michael Jordan, alikuwa miongoni mwa mastaa waliompa heshima kocha anayeondoka Manchester City, Pep Guardiola, katika sherehe yake ya kuaga klabuni hapo ambayo iliambatana na shamrashamra za aina mbalimbali kutoka kwa wanamuziki na wanamichezo wakiwamo wa michezo mingine nje ya soka.
Guardiola, 55, alitangaza wiki iliyopita kuwa anaaondoka Man City baada ya miaka 10 ya mafanikio makubwa, ambapo ameiongoza timu hiyo kushinda mataji 20.
Jordan, ambaye ni mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kuichezea Ligi ya Kikapu Marekani maarufu NBA, pamoja na nahodha wa zamani wa City, Vincent Kompany walikuwa sehemu ya wageni wa kushtukiza katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Co-Op Live mbele ya mashabiki 19,000 walionunua tiketi maalumu zilizouzwa na kumalizika ndani ya saa saba.
Kupitia ujumbe wa video uliochezwa ukumbini, Jordan alimzungumzia Guardiola akisema ni mmoja wa makocha bora waliowahi kuutumikia mchezo wa soka. “Nataka kukupongeza kwa kuwa na kazi ya kipekee sana, furahia kustaafu kwako. Kila la heri kwenye gofu na hakikisha mipira yako inakwenda sawa. Hongera,” amesema Jordan.
Guardiola anajulikana kutokana na kupenda mpira wa kikapu pamoja na mchezo wa gofu, ambapo katika nyakati za mapumziko amekuwa akitumia muda wake kuangalia michezo hiyo viwanjani na pia kucheza.
Naye mchezaji maarufu wa gofu Mwingereza Tommy Fleetwood alituma ujumbe wa pongezi kwa kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich na Barcelona akisema: “Unastahili kila jambo zuri utakalokwenda kufanya baada ya hapa. Ni heshima kukuita rafiki.”
Kocha mkongwe wa soka, Neil Warnock amesema: “Siwezi kuamini unaondoka. Nimewaona makocha wengi wakiondoka, lakini wewe uko juu kabisa. Wewe ndiye kocha bora zaidi niliyewahi kumuona.”
Mchezo wa mwisho wa Guardiola ulikuwa Jumapili ambapo Man City ilifungwa mabao 2-1 nyumbani na Aston Villa, huku Mhispania huyo akionekana akilia kwa hisia na mapema juzi, Jumatatu, maelfu ya mashabiki wa City walijitokeza katika mitaa ya Manchester kumuaga.
Mapema timu za wanaume, wanawake na akademi za Man City zilipita mitaani kwa mabasi kwenda Uwanja wa Etihad kabla ya kuelekea Co-Op Live kwa ajili ya sherehe ya mwisho ya kuagana na kocha huyo. Katika hafla hiyo, mshambuliaji wa timu ya wanawake wa City, Khadija Shaw alitangaza kwa mshangao kuwa amesaini mkataba mpya wa miaka minne kuendelea kubaki klabuni.
Watoto watatu wa Guardiola pamoja na wachezaji wa zamani Fernandinho, aliyekuwa mkurugenzi wa michezo Txiki Begiristain na kipa Ederson walibeba na kutembeza mataji yote 20 yaliyonyakuliwa na timu hiyo chini ya Guardiola.
Kocha wa sasa wa Bayern Munich, Vincent Kompany pamoja na kiungo Jack Grealish ambaye alikuwa kwa mkopo Everton msimu uliopita walipokewa kwa shangwe kubwa walipoonekana ukumbini, na katika hotuba yake ya mwisho akiwa na mwanamuziki wa Oasis, Noel Gallagher, Guardiola amesema: “Kwanza kabisa, asanteni sana kwa kuja kuniaga usiku huu. Usiku wa leo umeonyesha namna klabu hii ilivyo na mshikamano mkubwa. Asanteni sana. Sina maneno ya kutosha ya kushukuru. Kwa maisha yangu yote nitawabeba moyoni.”
Heshima pia zilitolewa kwa nahodha Bernardo Silva na beki John Stones ambao wataondoka klabuni mwishoni mwa mikataba yao msimu huu.
Akizungumza katika sherehe hiyo, mshambuliaji Erling Haaland amesema: “Ilikuwa furaha kucheza pamoja na Bernardo, John na bila shaka Pep. Tumeshinda mataji mengi. Bernardo na John ni wachezaji bora lakini pia ni watu wazuri. Imekuwa safari ya ajabu, lakini tunapaswa kuendelea kupambana hata bila wao.”