Mastaa hawa kuikamua Man United

Muktasari:
- Mastaa kama Marcus Rashford, Jadon Sancho, Antony, Alejandro Garnacho na Tyrell Malacia, ambao inataka kuwaondoa kwenye dirisha hili, wote kukosa timu za kuwanunua.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United huenda ikalazimika kutumia pesa nyingi sana kwenye dirisha hilo la usajili kuwalipa wachezaji ambao inataka kuwafungulia mlango wa kutokea, waondoke.
Mastaa kama Marcus Rashford, Jadon Sancho, Antony, Alejandro Garnacho na Tyrell Malacia, ambao inataka kuwaondoa kwenye dirisha hili, wote kukosa timu za kuwanunua.
Wachezaji wote hao, isipokuwa Garnacho tu walitolewa kwa mkopo na sasa wamerejea kwenye kikosi hicho wakati dili zao za mikopo zilipofika tamati mwishoni mwa msimu. Rashford, Antony na Sancho wote hawaonekani kwenda kuwa na maisha huko Old Trafford chini ya Ruben Amorim.
Garnacho aliwekwa kando kwenye kikosi kilichoanza fainali ya Europa League na siku za karibuni aliwatibua mabosi wake kwa kuvaa jezi ya Aston Villa akiwa mapumzikoni.
Lakini, wanunuzi au timu ya kuwabeba jumla wachezaji hao zimekuwa ngumu kujitokeza na Man United inataka kuachana na wakali hao wote.
Mikataba ya Garnacho, Rashford na Antony itafika ukomo 2028 - huku dhamira ya Man United kwa sasa ni kupunguza bili ya mishahara, hivyo inataka waondoke hata kama watakwenda kujiunga na wapinzani. Sancho naye atafunguliwa mlango wa kutokea licha ya kutolewa kwa mkopo kwenye misimu miwili iliyopita.
Rashford aliwekwa kando kabla ya kupelekwa kwa mkopo Aston Villa msimu uliopita. Kiwango chake kilikuwa kizuri huko na sasa mwenyewe anataka kwenda Barcelona, lakini shida miamba hiyo ya La Liha imeweka nguvu kwenye kumfukuzia Nico Williams.
Antony alionyesha kiwango bora kwa mkopo huko Real Betis, alipoisaidia timu hiyo kufika fainali ya Europa Conference League. Kuna uwezekano wa kubaki kwenye timu hiyo, ambayo ilikuwa ikilipa mshahara wake kwa asilimia 84. Kuhusu Garnacho, aliambiwa atafute timu ya kwenda na Chelsea na Napoli zimekuwa zikihusishwa na mpango wa kumsajili.
Man United iliwasajili wachezaji hao na kuwalipa mishahara mikubwa sana jambo linalowapa wakati mgumu kwa sasa kwenye kupata timu za kuwanunua, kwa sababu ya mishahara yao.