Mashabiki wamshangaza Amorim

Muktasari:
- Amorim ambaye hadi sasa ametimiza miezi minne tangu ajiunge na mashetani hao wekundu alisema moja kati ya kauli zinazomshangaza kutoka kwa mashabiki hao ni kumwambia kwamba anafanya kazi nzuri.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim ameshangazwa na maneno anayoambiwa na mashabiki wa Manchester United wanayomwambia kila wanapokutana naye.
Amorim ambaye hadi sasa ametimiza miezi minne tangu ajiunge na mashetani hao wekundu alisema moja kati ya kauli zinazomshangaza kutoka kwa mashabiki hao ni kumwambia kwamba anafanya kazi nzuri.
"Wananiambia jambo moja ambalo ni la ajabu kwangu: 'Unafanya kazi nzuri.' Ni vigumu kuelewa wakati mwingine lakini maneno hayo ni muhimu sana kwangu."
Kocha huyu raia wa Ureno tangu ajiunge na timu hii mambo hayaendi vizuri kwa upande wake akiwa ameshinda mechi sita tu na kupoteza nane kati ya 16 alizosimama kama kocha mkuu.
Kwa sasa timu hii inashika nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu England kwa pointi zao 33.
Licha ya kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki, Amorim, mwenye umri wa miaka 40, anakiri wazi kuwa katika nyakati zake za mwanzo alifanya makosa kwa kutoshirikiana vilivyo na wafanyakazi wengine kwenye timu hiyo.
Akizungumza na TNT Sports Amorim alisema:"Unapokuwa mchezaji unajiangalia wewe tu, lakini unapokuwa kocha unapaswa kuangalia watu wengi, sio wachezaji tu bali wafanyakazi wote.
"Wafanyakazi wote wanakutazama hivyo lazima umakinike kwa hilo, na hicho ni kitu ambacho sikufanya vizuri mwanzoni hapa Manchester kwa sababu nilikuwa nakiangalia zaidi masuala ya kiwanjani. Lakini kwa sasaninapata uhusiano mzuri sana na wafanyakazi wote na wachezaji."