Mashabiki waiponza Leeds United, FA yaanza uchunguzi
Muktasari:
- Taarifa ya FA imeeleza kuwa, chama hicho kimeanza kufanya uchunguzi huo, baada ya kujiridhisha kutokea kwa vurugu ambazo zilisababishwa na tabia ya hovyo ya mashabiki wa Leeds United ambao walichukizwa na matokeo ya mechi hiyo iliyomalizika kwa Tottenham kuibuka na ushindi wa mabao 1-2.
Chama cha Soka England (FA) kimeanza kufanya uchunguzi dhidi ya mashabiki wa Leeds United baada ya vurugu zilizojitokeza wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya EPL dhidi ya Tottenham iliyopigwa jana Jumamosi, Oktoba 04, 2025.
Taarifa ya FA imeeleza kuwa, chama hicho kimeanza kufanya uchunguzi huo, baada ya kujiridhisha kutokea kwa vurugu ambazo zilisababishwa na tabia ya hovyo ya mashabiki wa Leeds United ambao walichukizwa na matokeo ya mechi hiyo iliyomalizika kwa Tottenham kuibuka na ushindi wa mabao 1-2.
Pambano hilo lililokuwa na ushindani mkali, lilikuwa na matukio mawili tofauti ambapo vitu vilirushwa uwanjani na kuwafikia wachezaji wa Spurs. Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la Daily Mail, FA kimeanza kuchunguza matukio hayo, ambayo yanaweza kusababisha Leeds kutozwa faini kubwa.
Mchezaji wa kwanza kushambuliwa alikuwa Pedro Porro, ambaye alipigwa na kifaa cha kuvutia hewa chenye nikotini alipokuwa akisubiri kupiga kona. Kwa bahati nzuri, hakujeruhiwa, na alichukulia tukio hilo kama kebehi kutoka mashabiki hao.
Tukio la pili halikuwa la kuchekesha, kwani winga Mohammed Kudus nusura apigwe kichwani na chupa iliyorushwa kutoka kwa mashabiki.
Kudus alikuwa ameifungia Spurs bao la ushindi, na alipokwenda kushangilia kwa kuketi juu ya kigoda cha msimamizi mbele ya mashabiki wa Leeds, ndipo aliporushiwa chupa hiyo.
Katika video ya tukio hilo, inaonekana kitu kilirushwa kwa kasi kutoka kwenye umati na kilikaribia kumgonga Kudus pamoja na wachezaji wenzake waliokuwa wakimfuata.
Hakuna mchezaji aliyeonyesha hasira wala kuitikia tukio hilo kwa wakati huo, na kwa bahati nzuri hakuna aliyejeruhiwa.
Hata hivyo ilikuwa ni shangwe kwa kikosi cha Thomas Frank, ambacho kiliondoka Elland Road na alama zote tatu bila majeruhi.