Mashabiki wa Man United wavamia uwanjani

Muktasari:

MAELFU ya mashabiki wa Manchester United wamevamia kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa ajili ya kushinikiza mmiliki wa timu hiyo, familia ya Glazers kuachia timu yao.

MANCHESTER, ENGLAND. MAELFU ya mashabiki wa Manchester United wamevamia kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa ajili ya kushinikiza mmiliki wa timu hiyo, familia ya Glazers kuachia timu yao.

Mashabiki hao wenye hasira pia walizuia basi la wachezaji kuondoka kwenye Hoteli ya Lowry kwenda uwanjani kwa ajili ya kuvaana na Liverpool katika mchezo unaotarajiwa kupigwa leo pale Olds Trafford.

Mashabiki waliokuwa wakiandamana kwa amani walijikusanya nje ya uwanja huo wenye jina la utani la ‘Theatre of Dreams’ kwa ajili ya kushinikiza, wakati kocha Ole Gunnar Solskjaer akitaka maandamano yao yawe ya amani.

Lakini ghafla hasira ilionekana kupanda kwa mashabiki hao, walijikuta wakianza kurushiana makondo, wakati wengine wakirusha vitu vilivyofanana na fataki.

Katika picha za video, mashabiki hao walionekana wakilazimisha kuingia hadi katika eneo la kuchezea wakirusha fataki katika majukwaa huku wakipiga kelele kushinikiza familia hiyo ya Marekani kuachia timu yao.

Fataki hizo pia zilionekana kurushwa katika stuidio za matangazo za Sky Sports, eneo ambalo alikaa mchambuzi na mchezaji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher.

Sky Sports ilieleza katika matangazo yake kwamba kamera zao zilikuwa hatarini, kwani zilisukumwa na hata vibendera vya kona na vinasa sauti vingine vilichukuliwa na waandamanaji.

The Manchester Evening News iliripoti kwamba takribani mashabiki 10,000 walikuwa katika kampeni hiyo ya kuwaondoa Glazers, wakati wimbi kubwa la mashabiki likiwachoka wamiliki hao raia wa Marekani.