Mashabiki wa Brazil hatarini kukosa Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Marekani, Mexico na Canada zitakuwa wenyeji wa mashindano hayo yatakayofanyika mwakani kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 ambayo yatahusisha mfumo mpya wa timu 48.
NEW YORK, MAREKANI: MASHABIKI wa Brazil wanaotarajia kusafiri kwenda Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia la 2026 huenda wakakataliwa viza kutokana na sheria mpya zilizowekwa na nchi hiyo.
Marekani, Mexico na Canada zitakuwa wenyeji wa mashindano hayo yatakayofanyika mwakani kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 ambayo yatahusisha mfumo mpya wa timu 48.
Hata hivyo, hali hii inatokea wakati kukiwa na mvutano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Brazil.
Kwa mujibu wa CNN, Rais wa Marekani, Donald Trump, anafikiria kupiga marufuku utoaji wa viza kwa raia wa Brazil hata katika kipindi cha Kombe la Dunia.
Lourival Sant’Anna anadai kuwa maseneta wa Brazil walikumbana na masharti magumu ya visa walipotembelea Marekani wiki iliyopita, huku vikwazo hivyo vikiwa tayari vinatekelezwa.
Wanasiasa hao waliokuwa wakisafiri walipatiwa viza zenye masharti makali zaidi ya kawaida, hasa kuhusu idadi ya siku walizoruhusiwa kukaa Marekani.
Juni mwaka huu, Trump alipiga marufuku raia wa Iran kuingia nchini humo, akieleza kuwa ni kwasababu za kiusalama jambo ambalo linaweza pia kuathiri ushiriki wa timu na mashabiki wao katika Kombe la Dunia.
Hata hivyo, uamuzi huo hautawahusu wanamichezo au makocha wanaoshiriki mashindano ya kimataifa kama vile Kombe la Dunia au Olimpiki.
FIFA bado haijatoa tamko kuhusu suala hili, lakini rais wake Gianni Infantino ameonekana kuwa karibu sana na Trump katika wiki za hivi karibuni.
Wawili hao walikuwa wakionekana pamoja kwenye picha na video wakati wa Kombe la Dunia la Klabu lililopita ambalo pia lilifanyika Marekani.
Aprili mwaka huu, Trump alitangaza kuwa bidhaa kutoka Brazil zitatozwa ushuru wa asilimia 10 zinapoingia Marekani kiwango cha chini kabisa kinachotumika kwa nchi nyingi.
Lakini karibu miezi minne baadaye, ushuru huo umeongezeka hadi asilimia 50, na hivyo kufanya Brazil kuwa miongoni mwa nchi zinazotozwa ushuru mkubwa zaidi na Marekani duniani.