Mashabiki Spurs wamkataa De Zerbi
Muktasari:
- Kundi la mashabiki la Tottenham Hotspur Supporters’ Trust lilifanya mkutano wa dharura Jumatatu usiku na baadaye likawasiliana na klabu hiyo likisema haliwezi kuunga mkono uteuzi huo.
LONDON, ENGLAND: UPINZANI dhidi ya uteuzi wa Roberto De Zerbi kuwa kocha mkuu wa Tottenham Hotspur unaongezeka miongoni mwa makundi rasmi ya mashabiki, kutokana na kauli zake zenye utata alizowahi kutoa kuhusu Mason Greenwood.
Kundi la mashabiki la Tottenham Hotspur Supporters’ Trust lilifanya mkutano wa dharura Jumatatu usiku na baadaye likawasiliana na klabu hiyo likisema haliwezi kuunga mkono uteuzi huo.
Tottenham tayari imethibitisha kuwa De Zerbi, aliyewahi kufundisha Brighton na Marseille, ndiye atakayechukua nafasi ya Igor Tudor kwa mkataba wa miaka mitano.
Kundi hilo la mashabiki liliambia BBC kuwa limepokea malalamiko mengi kutoka kwa mashabiki kuhusu uamuzi huo. Pia, Ali Speechly, mmoja wa waanzilishi wa kundi la Women of the Lane, alisema wao pia wanapinga uteuzi huo na hataweza kuhudhuria mechi ikiwa De Zerbi ataendelea kuwa kocha.
De Zerbi aliwahi kusema kuwa Greenwood ‘amelipia kwa kiasi kikubwa’ baada ya kuondoka Manchester United kwenda Marseille, kufuatia kufutwa kwa mashtaka yaliyokuwa yanamkabili, ikiwemo jaribio la ubakaji na shambulio.
Greenwood alikamatwa mwaka 2022 akiwa mmoja wa wachezaji chipukizi waliokuwa na matumaini makubwa. Mashtaka yote yalifutwa mwaka 2023 na baadaye akaendelea na soka lake kwanza kwa mkopo Getafe kabla ya kujiunga na Marseille mwaka 2024.
Hata hivyo, kauli za De Zerbi zilionekana na baadhi ya mashabiki kama kupunguza uzito wa tuhuma hizo na kumwonyesha Greenwood kama mwathirika.