Mara Paap! Vardy katua Napoli
Muktasari:
- Vardy, 38, amekuwa hana timu tangu alipoachana na Leicester City mwishoni mwa 2024-25. Na licha ya kuhusishwa na klabu ndogo ndani na nje ya England, staa huyo wa zamani wa Three Lions, bado hana timu.
NAPLES, ITALIA: STRAIKA Jamie Vardy huenda akabamba dili matata kwenda kujiunga na Napoli ya Italia kutokana na mabingwa hao wa Italia kuhitaji saini ya mshambuliaji huyo asiyekuwa na timu kwa sasa.
Vardy, 38, amekuwa hana timu tangu alipoachana na Leicester City mwishoni mwa 2024-25. Na licha ya kuhusishwa na klabu ndogo ndani na nje ya England, staa huyo wa zamani wa Three Lions, bado hana timu.
Everton, Celtic na Rangers ni miongoni mwa timu zilizohusishwa na Vardy kipindi cha karibuni, huku mshambuliaji huyo akifunga mabao 200 katika mechi 500 alizocheza cha Leicester.
Lakini, Napoli imeonekana kutaka kufanya jambo kwenda kunasa saini ya Vardy wakati huu ikisaka Namba 9 mpya. Mabingwa hao wa Italia wanataka kuboresha safu ya ushambuliaji baada ya Romelu Lukaku kuripotiwa kwamba atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya paja.
Na baada ya Vardy kupatikana tu bure sokoni kwa sasa jambo hilo limeonekana kuivutia Napoli na kocha Antonio Conte. Napoli ina wachezaji wengine inaowasaka akiwamo straika wa Manchester United, Rasmus Hojlund na wa Chelsea, Nicolas Jackson, lakini wachezaji hao wawili watahitaji kulipiwa ada za uhamisho kutoka kwenye timu zao tofauti na Vardy.