Man United yaondoa jezi za mawinga sokoni

Muktasari:
- Lakini, miamba hiyo imeendelea kuchapisha jezi za winga mwingine, Mwingereza Marcus Rashford. Mawinga wote watatu walitumikia nusu ya msimu uliopita kwa mkopo.
MANCHESTER, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Manchester United imeziondoa sokoni jezi za mawinga wake Jadon Sancho na Antony sasa na kuziweka kando kwenye tovuti ya klabu hiyo.
Lakini, miamba hiyo imeendelea kuchapisha jezi za winga mwingine, Mwingereza Marcus Rashford. Mawinga wote watatu walitumikia nusu ya msimu uliopita kwa mkopo.
Sancho alikwenda Chelsea, wakati Antony alitamba kwenye kikosi cha Real Betis. Na Rashford kwa upande wake, alitumikia miezi minne huko Aston Villa baada ya kutibuana na kocha Ruben Amorim.
Kwenye duka la mtandaoni la Man United kumeonekana kuwa dalili, kuna uwezekano wa Rashford kurudi kikosini. Wakati ikiweka ubaoni jezi mpya za 2025/26, mashabiki walipewa chaguo la kununua jezi ya mkali huyo, “Rashford 10”.
Namba ya jezi ya Sancho imechukuliwa na kiungo Manuel Ugarte, wakati winga huyo alipokuwa akivaa Namba 25 kabla ya kupelekwa kwa mkopo Chelsea. Namba 21 iliyokuwa ikivaliwa na Antony kwa sasa ipo wazi, lakini haipo kwenye duka la mtandaoni la Man United la kuuza jezi za mastaa wake.
Rashford bado amebakiza miaka mitatu kwenye mkataba wake, wakati Antony mkataba wake utakwisha 2027 na Sancho amebakiza miezi 12 kwenye dili lake hilo la Old Trafford.
Rashford alianzishwa kwenye mechi mbili za kwanza chini ya kocha Amorim kwenye Ligi Kuu England na zote alifunga. Lakini, baadaye alijikuta akiwekwa kando na Mreno huyo, ambapo mechi yake ya alicheza Desemba 12 dhidi ya Viktoria Plzen kwenye Europa League. Baada ya kukaa benchi kwa wiki sita, Rashford alisaini kwa mkopo Aston Villa, ambako alifunga mabao manne na kuasisti sita katika mechi 17 chini ya kocha Unai Emery.
Kiwango chake kilimfanya atajwe na kocha Thomas Tuchel kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England.
Na kilichoelezwa ni kwamba Rashford alipanga kuzungumza hatima yake Man United katikati ya Juni.