Man United yamvutia kasi Valverde kumrithi Casemiro
Muktasari:
- Valverde, ambaye ni nahodha msaidizi wa Real Madrid, amejikuta katika hali ngumu baada ya tukio la ugomvi kambini kati yake na mwenzake Aurelien Tchouameni.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United inaripotiwa kuangalia uwezekano wa kufanya uhamisho wa kushangaza wa kiungo wa Real Madrid, Federico Valverde, ambaye anaonekana kuwekwa kando katika kikosi hicho cha Hispania kufuatia mzozo uliotokea katika uwanja wa mazoezi.
Valverde, ambaye ni nahodha msaidizi wa Real Madrid, amejikuta katika hali ngumu baada ya tukio la ugomvi kambini kati yake na mwenzake Aurelien Tchouameni.
Inadaiwa kuwa tukio hilo lilisababisha Valverde kuumia kichwani na kupata matibabu hospitali kutokana na mtikisiko wa ubongo (concussion), hali iliyomfanya akose mechi zilizosalia za msimu huu.
Baada ya tukio hilo, kiungo huyo wa kimatifa wa Uruguay alilazimika kutoa taarifa ya kuomba radhi hadharani, lakini bado inaelezwa kuwa viongozi wa Real Madrid wamekasirishwa na tukio hilo na sasa wanafikiria kumuuza katika dirisha lijalo la usajili.
Zaidi ya hapo, baadhi ya wachezaji wakongwe katika chumba cha kubadilishia nguo cha Real Madrid wameelezea kumuunga mkono Tchouameni na wanataka Valverde aondoke klabuni kabla ya msimu ujao.
Kutokana na hilo Manchester United wanafuatilia kwa karibu hali ilivyo huku wakiwa na nia ya kuimarisha safu ya kiungo katika dirisha la majira ya joto kutokana na kuondokewa na mastaa kadhaa akiwamo Casemiro ambaye pia alitua Old Traford akitokea Real Madrid.
United tayari wameonyesha nia ya kumsajili Tchouameni pia, lakini kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa anaripotiwa kutokuwa na mpango wa kuondoka Real Madrid kutokana na uungwaji mkono anaoupata ndani ya klabu.
Bado haijafahamika kama Valverde mwenye umri wa miaka 27 atakuwa tayari kuhamia Old Trafford, hasa ikizingatiwa kwamba ana mkataba na Real Madrid hadi 2029 na inaweza kuhitajika ada kubwa kiasi gani ya uhamisho.
Manchester United wameuweka usajili wa viungo wawili wa kiwango cha juu kama kipaumbele chao kikuu kutokana na kuondoka kwa Casemiro mwishoni mwa msimu na uwezekano wa kuuzwa kwa Manuel Ugarte, na miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa ni Elliot Anderson, Carlos Baleba, Adam Wharton, Tchouameni na sasa Valverde. Valverde ameichezea Uruguay mechi 73 za kimataifa na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha nchi yake katika Kombe la Dunia lijalo litakalofanyika Amerika Kaskazini.