Man United yaanza EPL kwa kipigo nyumbani
Muktasari:
- Man United iliyomaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 15, imejikita ikianzia hapo hapo msimu huu, licha ya kusajili washambuliaji wakali kikosini.
MANCHESTER, ENGLAND: Bao la dakika ya 13 kupitia kwa Riccardo Calafiori, lilitosha kuizima Man United katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya England (EPL) mbele ya Arsenal.
Man United iliyomaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 15, imejikita ikianzia hapo hapo msimu huu, licha ya kusajili washambuliaji wakali kikosini.
Wenyeji ikicheza kwenye Uwanja wa Old Trafford, jijini Manchester ilitawala sehemu kubwa katika mechi hiyo, lakini haikuweza kulikomboa bao hilo la Califiori.
Matokeo hayo yameifanya Man United kushika nafasi 15, huku Arsenal ikiwa ya sita katika msimamo unaongozwa na Manchester City baada ya raundi ya kwanza ya Ligi hiyo maarufu.
Klabu mbili za Leeds United iliyorejea EPL na Everton ndizo pekee ambazo hazishuka uwanjani wikiendi hii, kwani zitaumana kesho kukamilisha raundi ya kwanza.
Katika mechi za mapema, Chelsea ikiwa nyumbani jioni ilinusurika kipigo kutoka kwa mabingwa wa Ngao ya Jamii Crystal Palace baada ya V.A.R kulikataa bao la dakika 13 lililowekwa wavuni na Eberechi Eze.
Matokeo hayo yaliyotokea kwenye Uwanja wa Stanford Bridge, jijini London yameifanya Chelsea kufikisha mechi 17 bila kupoteza mbele ya Palace tangu 2017 kwa rekodi zinaonyesha imeshinda 14 na kutoka sare tatu mbele ya wapinzani wao hao wanaoshikilia taji la FA.
Nayo Nottingham ikiwa nyumbani iliishindilia Brentford kwa mabao 3-1.