Man United, Chelsea zakabwa koo EPL

Muktasari:

  • Chelsea ili kushiriki michuano ya kimataifa itatakiwa kuiombea Man United ipoteze mechi tatu na wao waendelee kushinda.

MANCHESTER United na Chelsea jana zilishindwa kufurukuta katika muendelezo wa Ligi Kuu baada ya zote kulazimishwa sare.

Man United ambayo ilicheza dhidi ya Brentford ilitoka sare ya bao 1-1, huku Chelsea iliyokutana Burnley ikitoka sare ya bao 2-2.

Matokeo hayo yalizidi kufifisha matumaini ya vigogo hawa kwenye mipango yao ya kushiriki  michuano ya Ulaya mwakani kwani tofauti ya alama dhidi ya timu zinazoshika nafasi ya kufuzu michuano hiyo inazidi kuwa kubwa.

Ah! Wamesawazisha!!? Rasmus Hojlund wa Manchester United akijiuliza baada ya Brentford kusawazisha bao katika dakika 89. United ilifunga bao lake dakika ya 86 katika sare ya 1-1 jana.

Chelsea ambayo ipo nafasi ya 11 kwa sasa ikiwa na alama 40 baada ya mechi 28, ili kufuzu michuano yoyote ya kimataifa itatakiwa kumaliza ndani ya nafasi sita za juu. Hadi sasa utofauti kati yao na Man United iliyopo nafasi ya sita ni pointi nane.

Kwa upande wa Man United ambayo inapambana kufuzu Ligi ya Mabingwa, kwa kumaliza ndani ya nafasi nne za juu, hadi sasa utofauti wa alama kati yao na Aston Villa iliyopo nafasi ya nne ni pointi 11.

Hivyo kwa upande wa Chelsea ili kushiriki michuano ya kimataifa itatakiwa kuiombea Man United ipoteze mechi tatu na wao waendelee kushinda.

Vilevile kwa upande wa Man United itatakiwa kuiombea mabaya Villa kwenye mechi nne huku wao wakishinda mechi zao.

Mbali ya mechi hizi, jana pia Tottenham ilishuka dimbani ikicheza dhidi ya Luton Town na kushinda mabao 2-1, Newcastle United nayo ikashinda mabao 4-3 mbele ya West Ham katika mechi ambayo Newcastle ilitanguliwa kwa mabao 3-1 kabla ya kupindua meza na kushinda 4-3.

Sheffield ikatoa sare ya mabao 3-3 na Fulham, Nottingham Foret ikiwa nyumbani pia ikatoa sare ya bao 1-1 mbele ya Crystal Palace, Bournemouth ikashinda mabao 2-1 dhidi ya Everton huku Villa ikiichapa Wolves mabao 2-0.