Man United, Brentford zakubaliana kwa Mbeumo
Muktasari:
- Man United ilishuhudia dili zake mbili zikikataliwa na Brentford, ikiwamo ya pili iliyokuwa ikizidi Pauni 60 milioni. Brentford iliendelea kung'ang'ania kulipwa Pauni 65 milioni kama malipo ya utangulizi na bonasi nyingine.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imefikia makubaliano na Brentford dili la kumsajili Bryan Mbeumo baada ya mazungumzo ya zaidi ya mwezi mmoja.
Man United ilishuhudia dili zake mbili zikikataliwa na Brentford, ikiwamo ya pili iliyokuwa ikizidi Pauni 60 milioni. Brentford iliendelea kung'ang'ania kulipwa Pauni 65 milioni kama malipo ya utangulizi na bonasi nyingine.
Lakini, ugumu wa kukamilika kwa dili hilo ulifika tamati baada ya klabu kukubaliana dili la Pauni 71 milioni, ambapo Man United italipa Pauni 65 milioni kwa awamu nne, kisha itaongeza Pauni 6 milioni kama bonasi kutokana na ubora wa mchezaji.
Mbeumo aliamua kuziweka kando klabu za Arsenal, Tottenham na Newcastle zilizoonyesha dhamira ya kumsajili na kuchagua kwenda kukipiga Old Trafford, licha ya kwamba Man United haitakuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Man United sasa itapambana kukamilisha dili hilo kwa wakati kabla ya ziara yao ya kwenda kwenye pre-season huko Marekani, Jumanne ijayo.
Huo utakuwa usajili wa pili wa mchezaji wa kikosi cha kwanza kufanywa na Man United kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya ule wa Matheus Cunha, ambaye alinaswa kwa ada ya Pauni 62.5 milioni kutokea Wolves.
Mbeumo alikuwa mmoja wa wafungaji mahiri kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, wakati alipotikisa nyavuni mara 20. Idadi hiyo ya mabao ilizidiwa na Mohamed Salah (29), Alexander Isak (23) na Erling Haaland (22) pekee.
Alihusika pia kwenye kuasisti, akifanya hivyo mara saba akiwa na kikosi cha Brentford.
Mbeumo anatarajia kwenda kucheza upande wa kulia wa Namba 10 kwenye fomesheni pendwa ya kocha Amorim ya 3-4-3, huku Cunha akicheza upande mwingine, nyuma ya Namba 9, ambaye inaelezwa kwamba ni usajili mwingine ambao Man United itafanya kabla ya dirisha hili kufungwa.
Kwingineko, Man United inaripotiwa kuwa kwenye mazungumzo ya kumsajili kipa wa Antwerp, Senne Lammens, 23, ambaye wanamtazama kama mtu wa kuja kuchukua mikoba ya majeruhi Andre Onana.