Makali ya Sesko gumzo
Muktasari:
- Sesko aliingia akitokea benchini na kufunga bao muhimu lililowapa Man United ushindi wa 1-0 dhidi ya Everton na kurejea katika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu England, usiku wa Jumatatu.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA, Michael Carrick ameambiwa hana ujanja zaidi ya kuanza la chaguo la straika Benjamin Sesko katika mechi ijayo ya Manchester United, hilo ni kwa mujibu wa Jamie Carragher.
Sesko aliingia akitokea benchini na kufunga bao muhimu lililowapa Man United ushindi wa 1-0 dhidi ya Everton na kurejea katika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu England, usiku wa Jumatatu.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 73.7 milioni kutoka RB Leipzig alikimbia karibu urefu wote wa uwanja kabla ya kumalizia kwa utulivu shambulizi la kushtukiza lililohusisha wachezaji wenzake wapya wa majira ya joto, Matheus Cunha na Bryan Mbeumo. Kwa kufanya hivyo na kushangilia kwa hasira baada ya bao hilo, alituma ujumbe wa wazi kwa Carrick.
Sasa Sesko amefunga mabao sita katika mechi saba zilizopita, huku mabao yake mawili ya karibuni yakiipatia Man United pointi nne muhimu, kufuatia bao la kusawazisha dakika za mwisho dhidi ya West Ham United.
Carrick amekuwa akimchagua Mbeumo kama mshambuliaji wa kati, akisaidiwa na Cunha, lakini Sesko anaendelea kubisha hodi kwa kiwango chake kizuri. Na kwenye hilo, Carragher alisema: “Sesko amekimbia zaidi ya mita 80 halafu akafunga, ungetarajia awe anapumua kwa nguvu baada ya juhudi hiyo, lakini bado alikuwa na nguvu za kushangilia kwa nguvu.
“Huenda alianza taratibu kuliko alivyotarajia mwanzoni, lakini hivi karibuni amekuwa moto sana. Tulikuwa tunajiuliza kama angeanza leo, sasa inaonekana ni jambo lisiloepukika. Amejipatia nafasi ndani ya kikosi.”
Sesko alifunga mabao mawili tu chini ya kocha Ruben Amorim, lakini sasa ameonekana kutulia na kung’ara chini ya Carrick licha ya kuingia kama mchezaji wa akiba. Carrick amefanya mabadiliko mawili tu katika mechi zake sita alizoongoza, yote yakisababishwa na majeraha, lakini Sesko anaendelea kumwekea presha kocha huyo wa muda.
Alipoulizwa kuhusu hamu ya Sesko kuanza kikosi cha kwanza, Carrick alijibu: “Ndiyo, kuna hilo kidogo. Lakini, si mara zote mambo yanakuwa makubwa kama yanavyoonekana. Naelewa kwa nini watu wanazungumzia hili sana. Lakini nina uhusiano mzuri sana na Ben. Tumekuwa na mazungumzo mazuri na yuko katika hali nzuri. Sehemu ya jukumu letu ni kumsaidia kupiga hatua katika maendeleo yake na kumkuza kama mchezaji.”