Mabadiliko Man United, Michael Carrick akipewa ‘rungu’
Muktasari:
- Vigogo wa klabu hiyo, chini ya uongozi wa Jason Wilcox na Christopher Vivell, tayari wamefanya uamuzi mzito kuhusu mustakabali wa timu hiyo inayojiandaa kwa msimu ujao utakaokuwa na mechi zaidi ya 40.
MANCHESTER, ENGLAND: BAADA ya matokeo ya suluhu mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Sunderland, Manchester United sasa imehamishia nguvu zake zote kwenye maandalizi ya msimu ujao. Huku timu hiyo ikiwa imejihakikishia nafasi ya tatu na kurejea Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Vigogo wa klabu hiyo, chini ya uongozi wa Jason Wilcox na Christopher Vivell, tayari wamefanya uamuzi mzito kuhusu mustakabali wa timu hiyo inayojiandaa kwa msimu ujao utakaokuwa na mechi zaidi ya 40.
Inaripotiwa kuwa, uongozi wa juu wa United umeshafanya uamuzi ya nani atakayekuwa kocha mkuu msimu ujao. Kocha wa muda na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Michael Carrick, ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kukabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Ili kupunguza mzigo mkubwa wa mishahara na kutengeneza nafasi ya usajili mpya, Manchester United inapanga kuwaachia baadhi ya nyota wake kama Casemiro ambaye atacheza mechi yake ya mwisho Jumapili hii dhidi ya Nottingham Forest, Jadon Sancho ataondoka kama mchezaji huru, Marcus Rashford na Andre Onana ambao kwa sasa wamewekwa sokoni kwa kiasi cha pauni milioni 1.125 kwa wiki kwenye bajeti ya mishahara.
Manuel Ugarte anatajwa kuwa kwenye mpango wa kuuzwa na Man United kwa pauni milioni 25.
Wakati wachezjai hao wakitajwa kuwa mbioni kuondoka, eneo la kiungo ndilo linalopewa kipaumbele kikubwa huku Kobbie Mainoo akionekana kubaki peke yake, ikidaiwa huenda akaungana na Aurelien Tchouameni anayewaniwa kutoka Real Madrid.
Hata hivyo, kuna wasiwasi juu ya utimamu wa mwili wa Lisandro Martinez na Matthijs de Ligt ambaye hatacheza tena msimu huu kufuatia majeraha ya mgongo tangu Novemba 2025.
Kwa upande wa makipa, Senne Lammens (23) anatarajiwa kuwa kipa namba moja, huku kijana Radek Vitek (22) aliyeng'ara kwa mkopo Bristol City akifikiriwa kubaki kama kipa namba mbili. Altay Bayindir anatarajiwa kurejea Uturuki.