Luis Enrique afunguka kumchapa Joao Pedro
Muktasari:
- Vurugu ziliibuka mwisho wa mechi baada ya The Blues kushinda 3-0, kasheshe lililohusisha pia wafungaji wa mabao Cole Palmer na Joao Pedro na staa wa PSG, Fabian Ruiz.
NEW JERSEY, MAREKANI: KOCHA wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique ameelezea kwa nini amemchapa kibao Joao Pedro kwenye vurugu zilizotokea baada ya Chelsea kushinda taji la Klabu Bingwa Dunia kwa kuifunga miamba hiyo ya Ufaransa 3-0 katika fainali iliyofanyika uwanjani MetLife, Jumapili.
Bosi huyo wa PSG, Luis Enrique alielezea kwa nini alimchapa kofi Joao Pedro, staa mpya wa Celsea.
Vurugu ziliibuka mwisho wa mechi baada ya The Blues kushinda 3-0, kasheshe lililohusisha pia wafungaji wa mabao Cole Palmer na Joao Pedro na staa wa PSG, Fabian Ruiz.
Presha ilikuwa kubwa baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo, na wachezaji walisukumana na kuvutanavutana. Makocha wa timu zote mbili walihusika baada ya Achraf Hakimi, Andrey Santos na Christopher Nkunku walipoonekana kupigana vipushi. Pedro alimfuata kocha Enrique, ambaye kwa hasira alijibu shambulizi hilo kwa kumchapa kibao Mbrazili huyo.
Kipa wa PSG, Gianluigi Donnarumma aliingilia na kumsukuma Pedro na kuanguka chini. Enrique alionekana kuwa mbogo wakati kocha Enzo Maresca alikuwa akiwaondoa wachezaji wake.
Lakini, Enrique alizungumzia jambo hilo, alisema: “Mwisho wa ile mechi kulitokea kitu ambacho naamini kingeweza kuzuiwa na kila mtu. Malengo na dhamira yangu, siku zote ilikuwa kuweka hali ya amani na si kuleta matatizo zaidi. Ni hali ya kuzuilika.
“Kulikuwa na hali ya kuhamaki, presha ilikuwa juu na watu walikuwa wakisukumana na nadhani sote tulipaswa kuzuia ile hali na hakika lile lisitokee tena. Lakini, nasisitiza dhamira yangu siku zote, ilikuwa kuweka hali ya utulivu kusiwe na matatizo makubwa.”
Balaa lote hilo lilikuja baada ya kiungo wa PSG, Joao Neves kuhamaki baada ya kipushi cha Marc Cucurella na kuamua kumvuta nywele tukio lililomfanya aonyeshwe kadi nyekundu dakika 85.