Lamine Yamal apewa namba 10
Muktasari:
- Staa huyo mwenye umri wa miaka 18 amechagua kutuliza daruga zake huko Nou Camp hadi 2031, huku akiwa ameshashinda mataji kibao na timu hiyo, ikiwamo LaLiga.
BARCELONA, ENGLAND: LAMINE Yamal amekabidhiwa jezi Namba 10 baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka sita kwenye klabu ya Barcelona licha ya kukabiliwa na kasheshe la kuajiri mbilikimo kwenda kutumbuiza sherehe za siku yake ya kuzaliwa.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 18 amechagua kutuliza daruga zake huko Nou Camp hadi 2031, huku akiwa ameshashinda mataji kibao na timu hiyo, ikiwamo LaLiga.
Yamal aliweka rekodi tamu kwenye kikosi cha Barcelona baada ya kufunga mabao 25 katika mechi 106. Umri wake mdogo haukumzuia winga huyo kuonyesha ubora wake.
Na Yamal ameweka jina lake kwenye vitabu vya kibabe vya michuano ya Euro huku akiitumikia timu ya taifa ya Hispania mara 20.
Na mkali huyo anayetumia mguu wa kushoto sasa amepewa dili la kuendelea kubaki Barcelona kwa miaka kibao kwa kusaini mkataba mpya. Na dili hilo limeongeza pia mshahara wake na kupandisha kiwango kilichowekwa kwenye mkataba wake kama kutakuwa na timu itahitaji kuvunja na kunasa saini yake.
Sambamba na dili hilo, Yamal amekabidhiwa jezi Namba 10, ambayo ilivaliwa na mastaa wa maana kabisa waliowahi kupita kwenye kikosi cha Barcelona ni Lionel Messi, Ronaldinho, Diego Maradona, Rivaldo, Romario na Hristo Stoichkov.
Jezi hiyo yenye Namba 10 ilikuwa wazi kwa Yamal kukabidhiwa baada ya Ansu Fati kuondoka kwenda Monaco.